Alhamisi, 18 Juni 2020

JAJI KAHYOZA: MBINU TULIZOJIWEKEA ZIMETUSAIDIA KUMALIZA MASHAURI KWA WAKATI.

Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha – Mahakama


Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma imefungua jumla ya mashauri 59 kati ya mwezi Machi na Juni mwaka huu ambapo kati ya hayo, mashauri 56 yalifunguliwa kwa njia ya mtandao (E-filling) na mengine matatu yalifunguliwa kwa njia ya kawaida.

Akizungumza na Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania  ofisini kwake hivi karibuni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza  alisema mashauri yaliyofunguliwa ni yale yenye Mamlaka ya awali “Original Jurisdiction” .

Jaji Mfawidhi alisema, mashauri mengi yaliyopokelewa  katika kipindi hicho ni  yenye Mamlaka ya Awali kwa ngazi ya Mahakama Kuu ni  ya mauaji ambayo ni mashauri 26, yanayotokana na migogoro ya ardhi 24 na madai tisa yaliyotokana shughuli za  uchimbaji wa madini migodini, yakiwemo ya  mikataba ya ajira na wafanyabiashara.

“Mashauri ya mauaji yamefunguliwa mengi  hasa kwa Wilaya ya  Tarime na migogoro ya ardhi inasababishwa na shughuli za kimaendeleo zinazoendelea hasa ujenzi wa miundombinu ya barabara kupita kwenye maeneo yanayomilikiwa na wananchi,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.

Mahakama imekuwa ikisisitiza umuhimu wa mashauri kumalizika kwa wakati ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi ambapo Kaulimbiu ya Maadhimisho ya  Wiki na Siku ya Sheria nchini  ya mwaka huu  inasema  “Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji,’’.

Akizungumzia maudhui hayo wakati wa kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Februari 6, mwaka huu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, alisema kuwa utawala wa sheria, na mfumo wa utoaji haki kwa wakati ni nyenzo muhimu katika kufanikisha na kurahisisha biashara, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.


‘‘Hivyo  tumekuwa  tukiweka mikakati na malengo mbalimbali ili tuweze kutoa huduma ya  utoaji haki kwa wakati ikiwa ni hatua ya  kuendana sambamba na kauli mbiu hii, ’ alisisitiza Jaji Kahyoza.

 Alieleza kuwa,wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutatua migogoro ya kiuchumi na biashara kwa kutumia njia mbadala ya usuluhishi na upatanishi “Alternative Dispute  Resolution” (ADR) kama sheria inavyoelekeza ili kuharakisha usikilizaji wa mashauri hayo. 

“Tumejiwekea lengo kwamba mashauri yote yenye Mamlaka ya Awali tunayoyapokea Mahakama Kuu tuyasikilize ndani ya miezi sita au kwa  yaliyoshindikana  kwa njia kusongezwa  hadi muda wa miezi tisa  badala ya utaratibu wetu wa kawaida wa miezi 24,” alisema.

Njia nyingine inayotumika kuharakisha usikilizaji wa mashauri  hayo ni kutoahirisha mashauri mara kwa mara,  ili mtu aweze kuahirishiwa  shauri  ni lazima awe na sababu ya msingi na nzito vinginevyo shauri lake linaondolewa mahakamani.

Jaji Kahyoza alifafanua kuwa, toka mwaka 2016 kulikuwa na masijala ya Mahakama ya  Kazi iliyokuwa ikipokea mashauri ya migogoro ya kazi kwa ngazi ya Mahakama Kuu kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 na kusajili  mashauri 144 baada ya kuanza kazi kwa Mahakama  hiyo,  walijiwekea mikakati ya kusikiliza na kuitolea maamuzi kabla ya kuisha kwa mwaka 2019, tulifanikiwa na kubakiwa na mashauri 30 hadi Juni mwaka huu.

Kwa upande wa Teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA), Jaji Kahyoza alisema Mahakama  hiyo  imepiga hatua kubwa kwa kutumia bajeti yao  ya ndani katika  kuhakikisha suala la matumizi ya  teknolojia hiyo linafanikiwa katika Mahakama nyingine zilizopo kwenye kanda hiyo.  Hivyo alisema wamesambaza vifaa  vya teknolojia kwenye Magereza ya Wilaya za Tarime, Serengeti na Bunda vya kuendeshea mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao  “Video Conference”, ruta  na kuwawezesha bando.

Alisema Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya zote wamewawezeshwa kwa kupatiwa kompyuta mpakato ili nao waweze kusikiliza mashauri kwa njia hiyo.

Mahakama  hiyo imepokea na kusajili mashauri yapatayo 471 kuanzia Januari hadi Juni 12,  mwaka huu na  Majaji wamefanikiwa kusikiliza na kutoa maamuzi kwa mashauri 398 kwa kipindi hicho.

Naye Mkuu wa Mkoa  wa Mara, Mhe. Adamu Malima, alimshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli na Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kuwapatia jengo la Mahakama hiyo kwa kuwa ni jambo kubwa ambalo linawezesha wananchi wanyonge kuifikia huduma na kupewa haki zao.

Aliongeza kwamba Mahakama hiyo itakuwa na manufaa kwa wana Mara wengi.
Kwa  upande  wake Mtendaji wa Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya alisema jengo hilo la kisasa limewasaidia kuboresha utendaji wa kazi kwa watumishi  kwa sababu kila mtumishi ana eneo lake la kufanyia kazi kwa nafasi na ufanisi.

‘‘Suala  la kupotea kwa majalada sasa limebaki kuwa historia,  tuna mfumo wa  kuhifadhi na kuyarudisha kwa wakati majalada,  pia  jengo hilo lina ghorofa mbili,  zenye  vyumba  vya ofisi 50, bado tuna nafasi za kutosha  hata kama Majaji  wa Mahakama ya Rufani Tanzania wakiwa wanafanya vikao vyao watafanya kazi bila bugudha. Hivyo tuko katika mazingira ya kazi ambayo ni rafiki, ’’ alisema Chonya.

Jengo hilo la kisasa  lina ofisi za wadau mbalimbali wa Mahakama, wakiwemo washauri, Wadau wa Haki Jinai na Madai.

Alisema ili Mahakama hiyo iendelee kutoa huduma za kisasa kulingana na hadhi ya jengo wanahitaji watumishi 30, ambapo kwa sasa waliopo  ni 34, hivyo mtumishi mmoja anafanya kazi zaidi ya moja ili kuondoa pengo hilo, mfano dereva  anafanya kazi pia ya kuwapokea wageni na kutoa msaada wanaohitaji.

Mtendaji huyo alisema ujenzi wa jengo hilo, umegharimu zaidi ya shilingi bilioni sita pamoja miundombinu iliyopo, na wana wajibu wa  kutunza rasilimali zilizopo  ili zidumu kwa muda mrefu  katika mazingira bora.

 ‘‘Tumejenga nyumba mbili za majaji ambazo zina miundombinu ya kisasa ya kumwezesha Jaji kufanya kazi akiwa nyumbani hata kwa kupitia Mahakama Mtandao, zenye thamani ya shilingi bilioni 1.5,’’ aliongeza Chonya.

Chonya  aliendelea kusema kwamba, kupitia Mahakama hiyo wameweza kutoa ajira ya kudumu  kwa watu 21, watano kati ya ni walinzi, waliobakia ni wanashughulika na usafi wa mazingira, ikiwa ni hatua ya kuwaongezea kipato.

Baadhi ya wakazi wa Musoma, ambao ni Bi. Moshi Zirang’esa na Bw.Deogratias Kimaro ambao awali walikuwa vibarua wakati wa ujenzi,  walishukuru kuwepo  jengo hilo ambalo limewasaidia kupata ajira ya kudumu ya mkataba wa mwaka mmoja , ambayo imewasaidia kupata kipato cha kulipia ada za shule na kutunza familia zao , kujenga nyumba, kufuga baadhi ya  mifigo ilikuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla, ikiwemo kupata uzoefu juu ya shughuli za kimahakama.

Wananchi waliofika kwa ajili  ya kupata  huduma  mahakamani hapo, walisema wameridhishwa nazo kwa kuwa zimewapunguzia gharama.

Waliiomba Serikali iweze kujenga majengo mengine kwenye maeneo mengine, ili kuwezesha wakazi wa maeneo hayo pia kupata haki kwa wakati na kuinua vipato vyao na kukuza uchumi na pato la taifa.

Awali wananchi wa mkoa huo, walikuwa wanapata huduma za Mahakama  Kuu  katika Jiji la Mwanza aqmbapo walilazimika kusafiri umbali wa kilomita 220 kupata huduma za Mahakama Kuu. Nauli kati ya Mwanza na Musoma kwa bus ni Shilingi 8,000 kwenda  tu, huku bado gharama  nyingine mfano za kurudi , malazi la chakula  kutegeamana na siku atakazotumia.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza akizungumzia kuhusu maboresho ya miundombinu ya Mahakama yalivyorahisisha utoaji haki.


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe.  Adam Kighoma Malima akizungumia kuhusu kuwepo kwa  baada ya Mahakama ya Tanzania kufanya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama yalivyorahisisha utoaji haki na kuokoa gharama kwa wananchi wa eneo hilo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma,  Bw.  Festo Chonya akizungumzia kuhusu maboresho ya miundombinu ya Mahakama yalivyorahisisha utendaji kazi kwa watumishi wa Mahakama hiyo.


 Msaidizi wa Kumbukumbu Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Bw,  Juma  Maiga akizungumzia utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali za Mahakama. 



Baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma katika  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.

 Kibarua aiyefanyakazi wakati wa ujenzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Bi. Moshi  Zerange’sa akielezea jinsi alivyopata ajira ya mkataba kwenye kampuni ya kufanya usafi mahakamani hapo.


 Baadhi ya vibarua waliofanyakazi wakati wa ujenzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, ambao pia wamepata ajira ya mkataba  wa muda wa mwaka moja kwenye kampuni ya kufanya usafi mahakamani hapo.


  Jengo la  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.

Jengo la  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.



                   Moja ya nyumba ya kuishi Jaji iliyojengwa katika kanda hiyo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni