Na
Lydia Churi-Mahakama, Dodoma
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema uhuru wa Mahakama
hauwezi kukamilika endapo watumishi wake hawatazingatia suala la uwajibikaji na
Maadili mema.
Akifungua
Mkutano wa Majaji wafawidhi na baadhi ya wajumbe wa kamati za Maadili
kuhamasisha ufahamu wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa
wa Mahakama jijini Dodoma, Jaji Mkuu amesema uhuru wa Mahakama usioambatana na Uwajibikaji na Maadili ni
uhuru ulio mashakani.
“Mwongozo
wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ni mfano wa hatua madhubuti
inayochukuliwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama katika kulinda uhuru wa Mahakama
na wakati huo huo kuimarisha Uwajibikaji na Maadili” alisema Jaji Mkuu.
Kifungu
cha 33(1) cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama (Sheria Namba 4 ya mwaka 2011
kimeipa Tume ya Utumishi wa Mahakama uwezo wa kukasimu utekelezaji wa majukumu
yake kwa Kamati zilioundwa chini ya Sheria hiyo ama zitakazoundwa na Tume.
Jaji
Mkuu alisema Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama utaisaidia
Tume hiyo kuzisimamia Kamati zilizokasimiwa mamlaka na pia utawezesha Kamati hizo
kuwa na utaratibu unaofanana katika kufikia maamuzi.
Alizitaja Kamati
zilizoundwa na Sheria Namba 4 ya mwaka 2011 kuwa ni Kamati ya Maadili ya Majaji
(Judges’ Ethics Committee), Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama (Judicial
Officers Ethics Committee), Kamati ya Maadili ya Mahakama ya Mkoa na Kamati ya Maadili
ya Mahakama ya Wilaya.
Alisema
Kamati za Maadili ngazi ya Mkoa na Wilaya zimebeba dhana ya kutegemeana (inter-dependence)
baina ya mihimili mitatu ya dola ili kuleta ufanisi katika shughuli za utoaji
haki.Aliongeza
kuwa katika kutegemeana na kushirikiana, kila Mhimili unapaswa kufahamu Mamlaka
na kazi za Mihimili mingine, kusaidiana, kulindana na kuteteana na Mihimili
kutoingilia au kuvamia au kuchukua kazi au majukumu ya mihimili mingine.
Alisisitiza
umuhimu wa Miongozo hiyo kusomwa na kueleweka ili iwasaidie Wahe. Majaji
Wafawidhi, Mahakimu wote, watumishi wote wa Mahakama, Wenyeviti wa Kamati, na
Wajumbe wa kamati za Maadili kutekeleza kwa vitendo dhana ya kutegemeana na
kushirikiana.
Kwa
mujibu wa Jaji Mkuu, Miongozo hii pia itaelimisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya
kufahamu majukumu ya Mahakama na kuhakikisha kuwa Kazi za Utoaji Haki
haziingiliwi.
Aliwataka
Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanapopokea malalamiko ya wananchi kuwaelimisha kuhusu
mipaka ya mamlaka na kuwashauri utaratibu wa kuwasilisha malalamiko yao kwa
mujibu wa sheria na taratibu.
Alisema
Miongozo hii inaweka mizani kwa Jaji, Msajili au Hakimu anapotimiza wajibu wake
kwa mujibu wa Katiba, Sheria na misingi ya kiapo chake, asiingiliwe, asibezwe
na asichukuliwe kuwa sio mzalendo hata pale uamuzi wake usipofurahisha. “Katika
mizani, Jaji, Hakimu au Msajili hawako juu ya Sheria. Katiba na Sheria zimeweka
utaratibu wa kupokea tuhuma dhidi ya viongozi hawa, kuzishughulikia, na hata
kuwaondoa katika utumishi wa Mahakama.
Waheshimiwa Majaji Wafawidhi wa Makama Kuu ya Tanzania kutoka kanda zote 16 nchini pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati za maadili walikutana kwa siku moja jijini Dodoma ili kujadili Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua Mkutano wa Majaji Wafawidhi na baadhi ya wajumbe wa kamati za Maadili kuhusu Uhamasishaji wa ufahamu wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama jana jijini Dodoma.
Baadhi ya Waheshimiwa Majaji wafawidhi wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi baada ya kufunguliwa kwa Mkutano |
Baadhi ya Waheshimiwa Majaji Wafawidhi na wajumbe wa kamati za Maadili wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi baada ya kufunguliwa kwa Mkutano
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni