Na
Lydia Churi- Mahakama Simiyu
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amesema uzuri wa
majengo ya Mahakama yanayojengwa hivi sasa hauna budi kuambatana na upatikanaji
wa huduma bora kwa wananchi.
Akizindua
jengo jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu pamoja na Mahakama ya wilaya ya
Bariadi, Jaji Kiongozi pia amewataka watumishi wa Mahakama nchini kubadili
mienendo na tabia zinazokiuka miiko na maadili ya kazi na Utumishi wa Umma ili
waweze kutoa huduma kwa ubora unaostahili.
“Natoa
Rai kwa viongozi wote kuhakikisha kwamba watumishi wote wa Mahakama wanatoa
huduma nzuri zinazoendana na uzuri wa majengo, tujiepushe na lugha zisizofaa
kwa wateja wetu ambao ni wananchi na wadau, tujiepushe na vitendo vya rushwa
kwani rushwa ni adui wa haki”, alisema.
Alisema
Mahakama haitasita kumchukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria mtumishi yeyote atakayebainika kujihusisha na
vitendo vya rushwa. Aliwaomba Wakuu wa Mikoa na Wilaya kupitia kamati za Maadili
ya Mahakimu kuwaelimisha wananchi
kutumia kamati hizi kuwasilisha malalamiko ya mienendo isiyofaa kwa baadhi ya
Mahakimu wanaokiuka maadili wanapotekeleza majukumu yao ya msingi ya utoaji
haki.
Jaji
kiongozi alisema uwepo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu ni nafuu na ukombozi
kwa wananchi wa Simiyu kwani awali walikuwa wakisafiri umbali wa kilometa 140
kwenda mkoani Shinyanga kufuata huduma za Mahakama. Alisema umbali huo mrefu
uliwaathiri kwa kutumia muda wao mwingi kutafuta haki na pia wengine waliikosa
haki kwa kukata tamaa na kushindwa kumudu gharama za kujikimu kwenda mkoani
Shinyanga.
Kwa
mujibu wa Jaji Kiongozi, moja ya mikakati iliyowekwa naMahakama ni kuhakikisha
kila eneo jipya la kiutawala linapoanzishwa inajengwa Mahakama kwa kuwa huduma
za Mahakama ni muhimu kama ilivyo huduma nyingine za Umma.
Wakati huo huo,
Jaji Kiongozi amewaomba wakuu wa mikoa nchini kuwezesha Magereza mikoani mwao kwa
kuipatia vifaa vya Tehama kwa ajili ya mikutano Mtandao (Video Conference) ili
kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania za kusikiliza
mashauri kwa njia hiyo.
Jaji
Kiongozi amesema Mahakama tayari imeweka mifumo ya Tehama kwenye mikoa
mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya mikutano mtandao na endapo wadau hao wa
Mahakama wataiwezesha Magereza, kazi hiyo itafanyika kwa urahisi.
“Wakati
Mahakama imejaribu kwa kiasi inachoweza kupeleka vifaa vya Tehama kwenye baadhi
ya Magereza, Mahakama sasa haiwezi kwasababu hatukuwa na bajeti, wadau wetu
mtuunge mkono kuwezesha Magereza kuwa na vifaa hivyo”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema
Magereza inakabiliwa na changamoto ya bajeti kwa ajili ya kununua vifaa hivyo pamoja
na vitendea kazi vingine yakiwemo magari ya kuwasafirishia mahabusu na wafungwa
kwenda mahakamani kwa ajili ya rufaa. Aliongeza kuwa baadhi ya wadau, huku
akimtolea mfano Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tayari wamepeleka vifaa vya Tehama kwenye
Magereza.
Jengo
la Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu lililozinduliwa ni la kisasa na shughuli
nyingi za kimahakama zitatumia mifumo ya Tehama baada ya kuunganishwa na Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano ambao utarahisisha matumizi hayo. Jengo hilo pia linajumuisha
Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya wilaya pamoja na ofisi za wadau kama vile
Waendesha Mashitaka, Ustawi wa Jamii, na Mawakili wa kujitegemea ambao
wametengewa vyumba vya ofisi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akifunia pazia kusoma maneno yaliyo kwenye kibao cha uzinduzi mara baada ya kuzindua jengo jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu ambalo pia linajumuisha na Mahakama ya wilaya ya Bariadi. Anayetazama ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga Mhe. Gerson Mdemu. |
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu ambalo pia linajumuisha na Mahakama ya wilaya ya Bariadi. |
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Mhe. Gerson Mdemu akizungumza. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Viongozi wa Serikali pamoja na Mahakimu wote wa Kanda ya Shinyanga mara baada ya uzinduzi wa jengo jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu ambalo pia linajumuisha na Mahakama ya wilaya ya Bariadi.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni