Na Magreth Kinabo- Mahakama
Kamati mpya ya Mafunzo na Utafiti ya
Jaji Mkuu wa Tanzania, leo imeanza kikao chake cha nne cha mwaka wa fedha wa
2019/2020 na kujadili majukumu mbalimbali ya kamati hiyo.
Akifungua kikao hicho cha siku mbili,
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Bethuel Mmilla alisema wana jukumu la kuongeza ushirikiano wa kuendelea kuleta
mageuzi katika maboresho yanayofanywa na
Mahakama ya Tanzania.
Kikao hicho kinafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Divisheni ya Ardhi, iliyopo Jijini Dar es Salaam.
‘‘Dhumuni kuu, la kuwa na kamati hii ni kuongeza ushiriki mpana ili mageuzi
haya tunayosimamia wenyewe yapate ushiriki wenu wa karibu zaidi na michango
bora, muhimu na itakayoleta ufanisi na tija kwenye Taasisi hii muhimu ya uendeshaji
wa nchi yetu,’’ alisema Jaji Mmilla.
Jaji Mmilla aliyataja baadhi ya majukumu ya kamati hiyo,
kuwa ni kufanya kazi kwa karibu na Idara ya Mafunzo, Idara ya Utafiti, Ufuatiliaji na Tathmini na Mkuu wa Chuo cha Uongozi
wa Mahakama Lushoto (IJA), kupitia Idara
ya Mafunzo endelevu iliyopo chuoni hapo kama kiungo, kupendekeza Sera ya
Mafunzo endelevu ya Maafisa wa Mahakama na wengine.
Majukumu mengine ni kushauri Baraza
la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA) moja kwa moja ama kupitia kupitia Mwenyekiti wa Baraza la Chuo au
wajumbe toka Mahakama, kuendekeza aina
mbalimbali za mafunzo endelevu, kumshauri Mkuu wa chuo cha IJA juu ya mahitaji
na vipaumbele vya Mahakama juu ya mafunzo endelevu.
Aidha aliongeza kwamba kamati hiyo itakuwa na kazi ya kufanya utambuzi na
kuwa na orodha ya Wakufunzi na vyuo kwa ajili ya mafunzo endelevu kwa viongozi
na watumishi wote kulingana na mahitaji na kufuatilia, kuchambua na kutathmini mafunzo mafunzo endelevu na mengine ya Maafisa
wa Mahakama wakiwemo wengine.
Kamati hiyo ina wajumbe saba, ambayo Jaji Mmilla, Majaji wa Mahakama ya
Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija na Mhe. Winifrida Korosso, wengine ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Lameck Mlacha, na Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe.Dkt. Benhaji Masoud na Mhe. Dkt. Modesta Opiyo, akiwemo Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe Dkt. Paul Kihwelo,
ambaye ni Mkuu wa chuo cha IJA.
Wajumbe hao waliteuliwa rasmi na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma Aprili 8, mwaka huu na watadumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha
miaka mitatu.
Kamati zingine zilizoundwa na Jaji Mkuu ni Kamati ya Kanuni, Kamati ya Takwimu na TEHAMA, Kamati ya Ufuatiliaji na Tathmini na Kamati ya Maboresho.
Baadhi ya Wajumbe wa
Kamati ya Mafunzo na Utafiti ya Jaji Mkuu wa Tanzania wakiwa kwenye kikao
hicho.
Wajumbe wa Kamati ya
Mafunzo na Utafiti ya Jaji Mkuu wa Tanzania wakiwa kwenye kikao hicho.
(Picha na Innocent Kansha- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni