Na
Innocent Kansha – Mahakama Tanga
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amepongeza Baraza la
Wafanyakazi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kusimamia utekelezaji
wa majukumu waliyopewa kisheria na miongozo iliyopo kwa ufanisi.
Akifungua kikao cha tatu
cha Baraza la tatu la Wafanyakazi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA),
Jaji Kiongozi alisema Mahakama ya Tanzania inaona fahari inapopata mrejesho
chanya wa namna ambavyo Chuo kinatekeleza majukumu yake kwa weledi.
Kwa mujibu wa Jaji Feleshi,
Chuo kimekuwa kikifanya vizuri katika eneo la utafiti na kimekuwa msaada mkubwa
kwa Mahakama katika masuala ya mafunzo na utafiti hivyo kuisaidia Mahakama ya Tanzania
kutekeleza kikamilifu wajibu wake wa kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati.
Aliwaambia wajumbe wa baraza
hilo kuwa Uongozi wa Mahakama unayo matarajio makubwa kwa chuo hicho chenye dhamana
ya kutekeleza sera ya mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 na mpango
wake wa miaka mitatu. Aliongeza kuwa Sera hiyo imeeleza bayana kuwa masuala
yote ya mafunzo kwa watumishi na tafiti zote zinazohusu Mhimili zitafanywa na
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
“Nawakumbusha watumishi
ambao hamjajiunga na chama chenu cha wafanyakazi mjiunge wakati ni huu ili
kwenda pamoja, mfaidike kwani lengo lenu ni moja tambueni hakuna haki bila
wajibu na haya mambo mawili yanaendana”, alisisitiza Jaji Kiongozi.
Jaji Feleshi aliwataka
wajumbe kutumia utaratibu wa kujadili mipango ya kuboresha miundombinu na
kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kuendesha mafunzo na
tafiti ikiwemo mafunzo kwa njia ya mtandao ambayo yamekifanya Chuo kuwa mfano kwa
ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Awali akimkaribisha mgeni
rasmi, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Paul Kihwelo alisema baraza hilo
limejumuisha watumishi wa kada zote walioajiriwa na chuo na limeundwa kisheria
na kwa kuzingatia matakwa ya Sheria za Kazi na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.
“Baraza hili ndiyo chachu
ya kuimarisha na kuongeza tija sehemu ya kazi kiutendaji, mafanikio ya Chuo
yanatokana na jitihada za Baraza hili katika kuboresha majukumu ya taasisi ya
kila siku, hii inatokana na lengo la ushirikishaji wa watumishi katika
uendeshaji wa Chuo”, alisema Jaji Kihwelo.
Baraza la Wafanyakazi wa
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto lilizinduliwa rasmi na Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Desemba 10 mwaka 2018 Mjini Dodoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.
Dkt. Eliezer Feleshi akihutubia wakati wa uzinduzi wa Kikao cha tatu cha Baraza
la tatu la Wafanyakazi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Kushoto kwake ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe. Amiri Mruma, wa pili
kulia ni Mwenyekiti wa Baraza na Mkuu wa Chuo cha IJA Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na
wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe.Edson
Mkasimongwa.
Mwenyekiti wa Baraza na
Mkuu wa Chuo cha IJA Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akizungumza wakati wa Baraza la wafanyakazi wa IJA, Kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe.Edson Mkasimongwa na wa
kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe.
Amiri Mruma.
Baadhi ya wajumbe wa
Baraza la tatu la Wafanyakazi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)
wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi wakati wa uzinduzi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni