Jumamosi, 25 Julai 2020

IJA WATAKIWA KUTUMIA FURSA KUKUZA IMANI KWA WADAU

Na Innocent Kansha – Mahakama, Lushoto.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameuwataka Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na watumishi kutumia fursa zilizopo kukuza imani kwa wadau wake katika utafiti, mafunzo na miongozo ya mafunzo ili kutoa elimu bora.

Akizungumza na Watumishi wa chuo hicho akiwa katika ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Tanga, Jaji Kiongozi alisema Mahakama ya Tanzania inakitegemea na kukiamini chuo hicho katika kutoa na kukuza viwango vya mafunzo na utafiti ulio bora.

“Ni wakati muafaka sasa chuo kiendelee kutoa mafunzo na elimu bora,  kuwe na uhuru wa kufanya tafiti katika maeneo ya kuboresha ili kutoa bidhaa zilizo bora zaidi katika ushindani wa soko la ajira na ustawi wa uchumi wa Taifa, alisema Jaji Kiongozi”.  

Alisema matarajio ya Mahakama ni makubwa kwa taasisi hiyo katika utoaji wa mafunzo na kuwa tafiti mbalimbali zinazofanywa ni za viwango vinavyokubalika. Aliongeza kuwa kwa upande wa watumishi, shuhuda mbalimbali zinaonyesha kuwa viwango vya chuo cha IJA ni vya juu kulinganisha na washindani wengine katika utoaji mafunzo na kufanya tafiti.

Dkt. Feleshi aliwakumbusha watumishi hao kushirikiana, kupendana na kuwa wawazi wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku na kuepuka kutumia pahala pa kazi kama sehemu ya kufanyia harakati zisizofaa.

Akizungumzia matumizi ya Tehama ndani ya Mahakama, Dkt. Feleshi alisema Mahakama inayo mifumo ya kurahisisha shughuli za utoaji wa haki na kuwataka wahadhiri pamoja na wanachuo kutembelea mifumo hiyo ili wapate taarifa muhimu za Mhimili na kutoa maoni, ushauri na hata mapendekezo ya kuboresha huduma za Mahakama.

Jaji Kiongozi leo amehitimisha ziara yake kwa mkoa wa Tanga baada  ya kutembelea chuo cha uongozi wa Mahakama Lushoto na kufanya mazungumzo na watumishi wa chuo, Wanachuo, Wajumbe wa Menejimenti na halmashauri tendaji ya chama cha wafanyakazi na Wanachuo.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Eliezer Feleshi  akizungumza kwenye kikao na watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA). Kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu Bi. Masalu Kisasila.

     Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Eliezer Feleshi (aliyeketi katikati) akiwa kwenye kikao cha watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) kilichofanyika kwenye Ukumbi wa hicho jana na kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu Bi. Masalu Kisasila.

 Baadhi ya Watumishi wa Chuo cha uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakiwa kwenye Kikao na  Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Eliezer Feleshi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Chuo hicho jana. 

    Wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Eliezer Feleshi. 


     Baadhi ya Watumishi wa Chuo cha uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakiwa kwenye Kikao na  Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Eliezer Feleshi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Chuo hicho jana aliyesimama ni moja miongoni mwa watumishi akiwasilisha jambo. 


(Picha na Innocent Kansha – Mahakama ya Tanzania)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni