Ijumaa, 24 Julai 2020

JIEPUSHENI NA USHABIKI WA SIASA: JAJI KIONGOZI

Na Innocent Kansha – Mahakama, Mkinga

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka watumishi wa Mahakama kujiepusha na ushabiki wa siasa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uhuru na kutenda haki.

 “Mjiepushe na mambo ya ushabiki wa vyama vya siasa hasa katika muda huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, tunatakiwa kutoa maamuzi tukiwa huru, haki yetu ya msingi ni kupiga kura na si vinginevyo”, alisema.

Jaji Kiongozi ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkinga akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Tanga ambapo alitembelea Wilaya Mkinga na kukagua miradi ya Mahakama inayotarajiwa kuanza kutekelezwa.

Miradi hiyo ni pamoja na jengo lililotolewa na Halmashauri ya Wilaya litakalo tumika kutoa huduma za Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo ya Mjini. Jaji Kiongozi pia alitembelea eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta saba litatumika kujenga Mahakama ya Wilaya ya Mkinga.

“Inaonekana kuna uhitaji mkubwa wa Mahakama ya wilaya na Mahakama za Mwanzo katika  wilaya ya Mkinga na ushahidi tosha ni kumuona Mkuu wa Wilaya akiwa pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama, kwa sababu kuanzishwa kwa dola na vyombo vyake ni kitu cha msingi kwenye kuimarisha ulinzi na usalama kwa ustawi wa wananchi” alisema.

 Jaji Kiongozi aliushukuru uongozi wa wilaya  kwa msaada na ushirikiano walioutoa kwa Mahakama ya Tanzania katika kuwasogezea karibu wananchi huduma za Mahakama kwa kuwa walikuwa wakizifuata mbali.

Aliongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2020 hadi 2021 ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Mkinga umeingizwa kwenye bajeti, hivyo mwakani kipindi kama hiki hatutazungumzia ujenzi bali kuanzisha huduma za utoaji haki ili kuungana na taasisi zingine za kiserikali ambazo zinaendelea kutoa huduma ndani ya Wilaya hii, alifafanua Jaji kiongozi.

Mahakama ya Tanzania kwa sasa imejiimarisha na inasisitiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufanya shughuli zake za kila siku za utoaji haki, mfumo huu umesaidia na kurahisisha uendeshaji wa mashauri na kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa kwa upande wa wadau na mahakama yenyewe, alieleza Jaji Kiongozi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga Bw. Yona Maki alipongeza juhudi na jitihada zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania za kuanzisha utoaji wa huduma za kimahakama katika wlayani ya Mkinga.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiangalia mchoro wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Mkinga linalotarajiwa kuanza kujengwa hivi karinuni.

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza  wakati alipomtembelea Mkuu wa wilaya ya Mkinga ofisini kwake.
  Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama. 
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wengine wa Mahakama. Wa tatu kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga Mhe. Amir Mruma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni