Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Watumishi wa
Mahakama ya Tanzania kufanya kazi kwa kujituma, kujitolea, na kushirikiana.
Akizungumza na
watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Kilindi jana wakati wa ziara yake ya kikazi
wilayani humo, Jaji Kiongozi pia amewataka watumishi hao kuzingatia maadili
wanapotekeleza majukumu yao ili kujenga taswira chanya ya Mahakama kwa wananchi.
“Ombeni kupewa kazi za
ziada kwa viongozi wenu pale mnapoona kituo husika hakina mashauri mengi, hata
kumsaidia Hakimu Mfawidhi kufanya utafiti ili kurahisisha kutoa maamuzi kwa
wakati au vituo vya jirani ili kuboresha utendaji”, alisema Jaji kiongozi.
Jaji Feleshi aliwashauri
watumishi kuanzisha vikao vya kitaaluma ili kujengeana uwezo katika fani zao.
Alisema Sheria na kanuni zimekuwa zikifanyiwa marekebisho mara kwa mara hasa
kwa miaka ya hivi karibuni ikiwemo sheria ya mwenendo wa madai na sheria za Mahakama
za mahakimu ili kutafuta na kupata ubobezi kwenye taaluma.
“Hakuna Hakimu wa mjini
wala wa kijijini wote nyinyi ni wamoja kwenye suala la kutafsiri sheria
zilizotungwa na Bunge na kanuni zake, vikao hivi vitawasaidia kuwajengea uwezo
na uelewa wa kuendesha shughuli zenu za kila siku za utoaji haki kwa wananchi”,
alisistiza Jaji Kiongozi.
Mhe. Jaji Feleshi
aliwahimiza watumishi kuzingatia maadili, kufanya kazi kwa bidii, na kuonyesha
uadilifu kwa vitendo waendelee kutenda haki. Aliwataka viongozi kusimamia
kikamilifu na kutumia busara katika kulea, kuonya, kutoa ushauri na kueleza
ukweli.
Aidha, Jaji Feleshi pia
amewataka viongozi kusimamia masuala yote yanayowahusu watumishi na kuyapa
kipaumbele ikiwa ni pamoja na kujenga mahusiano mazuri mahala pa kazi, kuzifahamu
changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati. Aliongeza kuwa endapo
viongozi watakuwa wakiwaelimisha watumishi haki zao za msingi watasaidia kuondoa
malalamiko yasiyo ya msingi.
Mhe. Dkt Feleshi aliwataka
watumishi kuendelea kuwahudumia wateja bila kuchoka na kuacha kutumia lugha
zisizofaa.” Wadau wetu wengi mara nyingi wanapofika mahakamani huwa na mitazamo
tofauti hivyo wakieleweshwa wataelewa na kuondoa migongano na manung’uniko
yasiyo ya lazima”, alisema.
Wakati
huo huo Jaji Kiongozi alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Kilindi
Bi. Sauda Mtondoo Ofisini kwake na viongozi wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya
wilaya na kufanya mazungumzo ambapo Mkuu huyo wa wilaya aliishukuru Mahakama ya
Tanzania kwa kuanzisha Mahakama ya Wilaya ya Kilindi baada ya maombi ya muda mrefu.
Akizungumza na Mkuu huyo
wa wilaya, Jaji Kiongozi alisema Mahakama kwa sasa imejiimarisha na inasisitiza
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kurahisisha shughuli
zake za kila siku za utoaji haki.
“Mfumo huu umesaidia kurahisisha
uendeshaji wa mashauri na kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa kwa upande wa
wadau na Mahakama, hivyo tembeleeni mifumo ya Mahakama ili kujua mambo mengi
yanayofanyika”, alisema.
Jaji Kiongozi pia alitembelea
eneo linalojengwa Mahakama ya Wilaya ya Kilindi na kupokea taarifa ya maendeleo
ya ujenzi wa jengo la Mahakama hiyo kutoka kwa Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania
Kanda ya Tanga.
Jaji Kiongozi ameanza
ziara ya siku tano Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga ambapo atakagua
shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.
Dkt Eliezer Mbuki Feleshi akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Mahakama ya wilaya ya Kilindi kuanza ziara yake ya kikazi katika kanda ya Tanga.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi (kulia) akiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe. Amir Mruma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza alipomtembelea Mkuu wa wilaya ya Kilindi Bi. Sauda Mtondoo ofisini kwake. Jaji Kiongozozi yuko Tanga kwa ziara ya kikazi.
Jaji
kiongozi wa Mahakama kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi
wa Mahakama ya Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga. Wa nne kushoto ni Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe. Amir Mruma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga na Mahakama Kuu ya Tanzania na Viongozi wa
kamati ya ulinzi na Usalama ya wilaya ya Kilindi. Wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Sauda Mtondoo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe. Amir Mruma akizungumza.
Jaji kiongozi wa Mahakama kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Kilindi (hawapo pichani)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni