Na
Innocent Kansha-Mahakama Rombo
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amemuelezea
aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora Marehemu
Jaji Salvatory Bongole kuwa alikuwa ni mtu mnyenyekevu, mtiifu na mchapakazi katika
utumishi wake siku zote wakati wa uhai wake.
Jaji
Kiongozi jana aliwaongoza Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Watumishi wengine
wa Mahakama, viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi wa wilaya ya Rombo
katika mazishi ya Jaji Bongole yaliyofanyika kijijini kwao Shimbi Kati wilayani
Rombo mkoani Kilimanjaro.
Akitoa
salaam za rambirambi kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania, Dkt. Feleshi alisema
maisha ni kama kitabu ambacho kawaida huwa na mwanzo na mwisho wake hivyo
umefika wakati wa kusherehekea mwisho wa maisha ya Jaji Bongole.
“Natoa
salaam za pole kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
ambaye kutokana na majukumu mengine hakuweza kuhudhuria mazishi haya”, alisema
Jaji Kiongozi.
Alisema
kama wanadamu hatuna budi kujifunza kuhesabu siku za maisha yetu tuwapo hai na
kutenda matendo ya uadilifu katika majukumu ya kila siku. Alisema Marehemu Jaji
Bongole, alikuwa ni rasilimali kubwa na muhimu kwa Mahakama kwa kuwa katika
vituo mbalimbali alivyohudumu alishiriki katika mageuzi makubwa kwa maslahi ya
mhimili na taifa kwa jumla.
Alisema,
kutokana na kuaminiwa kwake, alipokuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi alishiriki
kikamilifu katika ujenzi wa Mahakama kuu Iringa, Mahakama ya Hakimu Mkazi na
Mahakama ya wilaya ya Iringa, maarufu kama (Iringa Judiciary Square) ambayo kwa
sasa ni sehemu ya mfano katika Mahakama kwani imesaidia kwa kiasi kikubwa
katika suala zima la utoaji haki kwa wananchi.
Jaji
Kiongozi alisema Jaji Bongole pia alishiriki katika ujenzi wa Mahakama Kuu
kanda ya Sumbawanga, Mahakama za wilaya ya Ludewa za Mbarari Sumbawanga Njombe
na Mahakama za Mwanzo za Iringa, Rujewa na Mlowo. Pia alisimamia ujenzi wa
majengo ya Mahakama Kuu Shinyanga, Mahakama ya wilaya ya Bukombe na Mahakama za
Mwanzo za Mwandiga, Mabamba Ilolangulu na Mwadui.
Naye
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alimuelezea Jaji Bongole kuwa alikuwa ni
mtumishi mwenye moyo wa kujituma, msikivu, mnyenyekevu na aliyependa
kushirikiana katika kazi zake siku zote. Aliongeza kuwa Jaji Bongole pia
alikuwa hodari, mchapakazi, mcheshi na mshika dini aliyemtanguliza Mungu katika kazi zake na mwenye sifa za kuigwa katika jamii iliyokuwa inamzunguka.
Wakati
huo huo, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora Mhe.
Khamis Amour alimuelezea Jaji Bangole kuwa ni mtu aliyekuwa mahiri na
kutanguliza mbele maslahi ya watu aliowahudumia na kuwa Mahakama imepoteza
mwalimu, rafiki na mlezi mzuri.
Jaji
Amour alisema marehemu alikuwa ni mwenye utashi aliyechukua changamoto na
kuzigeuza kuwa fursa na kuzitatua ili kazi ziweze kufanyika kwa njia bora ya na
kisuluhishi kwa kuwa alikuwa ni mtaalamu wa eneo hilo.
Jaji
Salvatory Bongole alifariki dunia siku ya Jumatano Julai 15, 2020 usiku baada
ya kuugua ghafla nyumbani kwake.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.
Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza wakati wa Mazishi ya aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania kanda ya Tabora Marehemu Jaji Salvatory Bongole.
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye Mazishi ya aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora Marehemu Jaji Salvatory Bongole.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiweka shada la Maua kwenye kaburi la aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora Marehemu Jaji Salvatory Bongole baada ya mazishi yake.
Watoto wa Marehemu Jaji Salvatory Bongole wakiweka shada la Maua kwenye kaburi la baba yao mara baada ya mazishi yake.
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakishuhudia mazishi ya aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora Marehemu Jaji Salvatory Bongole. Pichani Jeneza lenye mwili wa Marehemu likiwa tayari kushushwa kaburini.
Apumzike kwa amani
JibuFuta