Jumatano, 1 Julai 2020

UBORA WA JENGO LA MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA UKIDHI HADHI YA MUHIMILI

Na Innocent Kansha- Mahakama
Mahakama ya Tanzania leo  imesaini mkataba wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama baina yake na Kampuni ya Reli kutoka China CRJE (EAST AFRICA) kwa makubaliano ya kukabidhi kazi hiyo ndani ya miezi 24.

Hafla hiyo imefanyika katika ofisi za makao makuu ya Mahakama Jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia kuhusu mkataba huo,  Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru alisema anategemea muda waliokubaliana wa kupokea jengo hilo utakuwa kwa wakati muafaka na  litaendanana na hadhi ya Muhimili husika.

‘‘Nategemea kuona tunapokea jengo zuri lenye ubora halisi unaoendana na thamani ya mkataba huu, kwani Mahakama ni moja ya nguzo ya Serikali hivyo hatutarajii kuona jengo lisilo lingana na hadhi ya Muhimili wenyewe,’ alisema Kabunduguru.

 Aliongeza kuwa Mahakama ina wajibu wa kuhakikisha kila mtu anapata haki sio kwa Watanzania tu hata kwa wageni wanaofika hapa nchini kwa shughuli mbalimbali ikiwemo uwekezaji na Muhimili huo unatarajia kuwa na  jengo hilo liwe chachu ya uharakishaji wa utoaji haki kama ilivyo  katika jukumu  lake la msingi la kikatiba.

Mtendaji huyo aliitaka  ofisi ya Wakala wa Usimamizi wa Majengo Tanzania (TBA) itambue kwamba  inayo wajibu  wa kusimamia ujenzi huo sio kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania bali kwa niaba ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani Mahakama ni sehemu ya kiungo au Muhimili wa Serikali.

‘Mkandarasi unayo kazi kubwa mbele yako ya kuhakikisha unatekeleza wajibu wako ipasavyo ili uweze kupimwa kwa thamani ya jengo hili.

‘‘Niwakumbushe tu kwamba leo hii tumeingia kwenye jukumu kubwa na zito la kutia saini ujenzi huu tunategemea kuona sio tu kazi iliyo bora bali kazi inayotazamwa na Taifa zima kwa ujumla, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha ujenzi huu unafanikiwa kwa kiwango kinachokidhi hadhi ya Mahakama,’’ alisisitiza.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Reli ya Nchini china CRJE (East Africa) Bw. Xie Zhixiang alihihakikishia Mahakama kuwa kampuni yao ina uzoefu mkubwa katika kutekeleza miradi mikubwa ya aina hii, hivyo wanategemea kujenga kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu kulingana na makubalianao ya ujenzi huo.

Kwa upande wa Mkandarasi Mashauri, Wakala wa Majengo Nchini (TBA), ambaye Msanifu wa Majengo Bw. Geofrey Munyaga alisema tunashukuru kwa kuaminiwa na serikali tupo tayari kutekeleza jukumu letu kikamilifu kama wasimamizi washauri katika mradi wa ujenzi huu tutahakikisha tunasimamia ubora wa ujenzi wa jengo hili unatekelezwa kama ilivyo kusudiwa na Serikali.

Mkataba wa ujenzi  huo, umeanza leo na utakamilika ndani ya miaka miwili.

 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru (katikati) leo  amesaini mkataba wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania  na  Mwenyekiti wa Kampuni ya Reli kutoka nchini China, Bw.Xie Zhixiang CRJE(East Africa) ambaye  hayupo pichani .Jengo hilo litajengwa kwa  muda wa miaka miwili, eneo la NCC Jijini Dodoma.( Kushoto) ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na (kulia) ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Kevin Mhina.



Mwenyekiti wa Kampuni ya Reli kutoka nchini China, Bw.Xie Zhixiang CRJE (East Africa) akisaini mkataba huo. Tukio hili limefanyika kwenye ofisi za  Makao Makuu ya Mahakama ya  Tanzania,Jijini Dar es Salaam.



Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru (katikati) leo  akikabidhi  mkataba wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama kwa  Mwenyekiti wa Kampuni ya Reli kutoka nchini China, Bw.Xie Zhixiang CRJE(East Africa).Jengo hilo litajengwa kwa  muda wa miaka miwili, eneo la NCC Jijini Dodoma.( Kushoto) ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na (kulia) ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Kevin Mhina.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru (kushoto) leo  akimwonesha  mchoro  wa jengo hilo, Mkandarasi Mshauri kutoka   ofisi ya Wakala wa Usimamizi wa  Majengo Tanzania (TBA), Bw.Geofrey Munyaga.


Mwanasheria wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Peace Mpango aweka saini mkataba huo.Wengine ni baadhi ya viongozi wa Mahakama, wakiwemo watumishi na wageni waalikwa.

(Picha na  Innocent Kansha – Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni