Na
Catherine Francis – Mahakama Kuu, Arusha
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru amewaasa watumishi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha kufanya kazi kwa kufuata kanuni na sheria
za utumishi wa Umma ili waweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani
Arusha hivi karibuni, Mtendaji Mkuu
Aliwataka watumishi kuachana na tabia zinazoashiria
rushwa na badala yake wawahudumie wateja pasipokuwa na malalamiko na
ucheleweshwaji wa huduma.
“Njia pekee ya kujiepusha na vitendo vya
rushwa na ukosefu wa maadili ni kutoa huduma bora pasipo upendeleo wala ubaguzi
wowote kwa wateja wote wa Mahakama ambao ni wananchi”, alisema.
Aidha,
aliwakumbusha kuwa ili kuweza kufanya kazi vizuri ni muhimu kuelewa asili ya
maeneo wanayofanyia kazi ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima kati ya
wateja wa Mahakama na watumishi wa Mahakama wanaotoa huduma. Aliongezakuwa kuna
baadhi ya migogoro hutokea kwa kutokuelewa uhalisia wa jamii inayokuzunguka na
mazingira yao.
Pamoja
na hayo aliwahamasisha watumishi kujiendeleza kielimu kutokuridhika na viwango
vya elimu walivyoingia navyo kwenye ajira.
Wakati
huo huo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewahimiza waheshimiwa
Mahakimu kutoa hukumu zilizo bora pasipo woga kwa kuwa wamepewa mamlaka hayo na
wanapaswa kuyatumia kwa ujasiri kwenye kutoa maamuzi yao.
“Lakini
pamoja na kuwa na ujasiri wa kutoa hukumu mnapaswa kuzingatia haki na sheria za
nchi katika kufanya maamuzi hayo kwasababu Mahakama ni Mhimili unachangia
katika usalama wa nchi.
Msajili
Mkuu aliwapongeza Mahakimu hao kwa kasi ya kusikiliza na kumaliza mashauri yaliyoko
mahakamani na kuwasisitiza kuhakikisha wanatoa nakala za hukumu kwa wakati ili
kupunguza malalamiko kwa wananchi.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania walifanya
ziara ya kikazi Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha Julai 15, 2020 ambapo
pia walipata wasaa wa kuzungumza na watumishi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru (wa pili kulia) akisalimiana na baadhi ya watumishi
wa Mahakama Arusha mjini mara baada ya kuwasili.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru (kulia), Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert
Chuma (katikati) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Bw. Edward Mbara wakisikiliza
hoja za watumishi.
Baadhi
ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha waliohudhuria kikao baina yao na Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni