JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAHAKAMA
TAARIFA
KWA UMMA
JAJI BETHUEL MMILLA AFARIKI DUNIA
DAR ES SALAAM, 25.09.2020
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma anasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Marehemu Jaji Bethuel Mpakani Kasefu Mmilla aliyefariki dunia usiku wa Septemba 24, 2020.
Kwa mujibu wa Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi
amesema, Marehemu Jaji Mmilla awali alilazwa katika Hospitali ya Jeshi ya
Lugalo Septemba 23, 2020 alipokuwa akipatiwa matibabu na baadae alihamishiwa
katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Marehemu Jaji Mmilla alizaliwa Septemba 22, 1956 katika Wilaya ya Makete
mkoani Njombe. Mnamo mwaka 1964 hadi 1970 marehemu alisoma shule ya Msingi Iniho
Wilaya ya Makete. Alijiunga na elimu ya
Sekondari mwaka 1971 hadi 1974 katika Shule ya Sekondari Lugalo iliyopo mkoani
Iringa, mwaka 1975 hadi 1976 aliendelea na elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari
ya Ilboru mkoani Arusha.
Aidha, Mwaka 1980 hadi 1983 marehemu Jaji Mmilla alijiunga na Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam ambapo alisomea Shahada ya kwanza ya Sheria (LLB). Alishiriki
pia katika kozi mbalimbali fupifupi.
Marehemu Jaji Mmilla aliajiriwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) Machi
21, 1978 ambapo alifanya kazi hadi mwaka 1980. Mwaka 1983 alifanya kazi Ofisi
ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali. Mnamo Februari 1984 Marehemu Jaji Mmilla
aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania kama Hakimu Mkazi ambapo alifanya kazi
katika vituo mbalimbali hadi Aprili, 1995.
Akiwa ndani ya Mahakama aliteuliwa pia kushika nafasi ya Usajili kazi
aliyoifanya hadi Juni, 2000. Kwa upande
mwingine, mwaka 2000 marehemu aliteuliwa kuwa Katibu wa Tume ya Kurekebisha
Sheria ambapo alifanya kazi hadi Juni, 2002.
Juni 05, 2002 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati
Benjamin William Mkapa alimteua marehemu kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania
ambapo aliitumikia Mahakama Kuu hadi Oktoba, 2012 alipoteuliwa kuwa Jaji wa
Mahakama ya Rufani hadi umauti unamfika.
Marehemu Jaji Mmilla atakumbukwa kwa uchapakazi na ushirikiano wa hali
ya juu.
Kwa mujibu wa Bw. Nyimbi amesema kuwa msiba upo nyumbani kwa marehemu
Mikocheni-Dar es Salaam na mipango ya mazishi itajulikana pindi
itakapokamilishwa.
BWANA AMETOA, BWANA
AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE.
Imetolewa
na:-
Mary C. Gwera,
Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
MAHAKAMA
YA TANZANIA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni