Na Mary Gwera, Mahakama
Mahakama
ya Tanzania ipo katika mchakato wa maandalizi ya kuadhimisha miaka 100 ya
Mahakama Kuu nchini tangu kuanzishwa kwake.
Kwa
mujibu wa Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt alisema
kuwa sherehe za maadhimisho hayo zitaanza mwishoni mwa mwaka huu (2020) na
kufikia kileleni mapema mwaka 2021.
“Mahakama Kuu ya Tanzania, ilianzishwa
kisheria 1920 na kuanza kufanya kazi rasmi Januari 03, 1921 ikiwa na masjala
chache,” alieleza Mhe. Sarwatt.
Msajili
huo alisema kuwa kupitia maadhimisho hayo, Mahakama itafanya shughuli
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuelimisha wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya
habari.
Aidha,
Mhe. Sarwatt alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa ngazi hiyo ya Mahakama nchini
kumekuwa na mafanikio kadhaa ikiwemo ongezeko la Masjala 22, Kanda 16 za
Mahakama Kuu, Divisheni nne (4) pamoja na Kituo cha Usuluhishi.
Mbali
na hilo, Msajili huyo aliongeza kuwa kumekuwa na mafanikio pia katika suala
zima la usikilizaji/uondoshaji wa mashauri, ongezeko la majengo ya kisasa,
Matumizi ya TEHAMA Mahakamani na kadhalika.
“Lengo
la Mahakama Kuu ni kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi, hivyo mpango
wa Mahakama ni kuwa na Mahakama Kuu katika kila mkoa,” alisisitiza Mhe.
Sarwatt.
Mahakama
ya Tanzania imegawanyika katika ngazi kuu tano ambazo ni Mahakama za Mwanzo,
Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi/Mkoa, Mahakama Kuu na Mahakama ya
Rufani.
Aidha, Mahakama Kuu ina Divisheni zake ambazo ni Mahakama Kuu- Divisheni ya Ardhi, Mahakama Kuu-Divisheni ya Biashara, Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi na Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi almaarufu kama Mahakama ya Mafisadi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni