Jumatano, 30 Septemba 2020

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA AITAKA KAMATI KUSIMAMIA RASILIMALI KWA UBORA UNAOTAKIWA

 Na Innocent Kansha – Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru amezindua Kamati mpya ya Ukaguzi wa Mahakama ya Tanzania na kuwataka wajumbe kusimamia rasilimali nyingi ilizonazo Mahakama ili iweze kufanya kazi katika ubora unaotakiwa.

Akizindua kamati hiyo leo jijini Dar es salaam, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania amesema sheria ya Fedha ya mwaka 2001 inampa mamlaka Mkuu wa Taasisi kuteua wajumbe wanne wa kamati ya ukaguzi na pia inatoa fursa kwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kuteua mjumbe mmoja.

“Nina imani tutaichukulia kamati yenu kama sehemu ya menejimenti, shabaha kubwa ikiwa ni kuhakikisha usimamizi wa rasilimali za Taasisi na mali za Umma zinalindwa na kusimamiwa kwa weledi mkubwa zinatumika vizuri na kudhibitiwa”, alisistiza Mtendaji Mkuu.

Alisema Kamati ya ukaguzi ni chombo cha utawala (Management Control System) kinachopewa jukumu la usimamizi wa Taasisi hasa kwenye mambo hatarishi, na kuhakikisha kuwa michakato ya udhibiti imeundwa na inafanya kazi kama ilivyo kusudiwa ili kufikia malengo.

Mtendaji Mkuu alisema kutokana na dhamana na umuhimu wa kamati hiyo, shughuli zake zinapwaswa kujumuisha wajumbe wa nje ili kufanya wajumbe waweze kufanya maamuzi sahihi yasiyokuwa na upendeleo.

“Kutokana na muundo huu ni matarajio yangu kwamba kamati itatekeleza wajibu na majukumu yake kwa uwazi na kuwezesha mamlaka ya ndani ya Mahakama kuchukua hatua stahiki kwa wakati kabla madhara hayajatokea”, alisema Bw. Kabunduguru.

Bw. Kabunduguru amemtaka Mkaguzi Mkuu wa ndani na timu yake kuhakikisha taarifa za ukaguzi wa ndani zinapatikana kwa wakati ili kushirikisha wadau wengine kutenda kazi zao kwa wepesi na uwazi zaidi kwakuwa wao ndiyo kioo cha Taasisi.

Mtendaji Mkuu aliainisha baadhi ya majukumu ya kamati hiyo kuwa kuimarisha shughuli za ukaguzi wa ndani na wa nje, ambapo ripoti zao kwa kamati ni chanzo kikuu cha mafanikio ya Taasisi.

Kamati hiyo pia inalo jukumu la kupitia na kupitisha mpango wa mwaka wa ukaguzi wa ndani pamoja na kupitia ripoti za ukaguzi wa ndani wa kila robo mwaka ili kuona changamoto zilizojitokeza na kuchukua hatua stahiki.

Majukumu mengine ya kamati ya ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania ni kupitia mkakati wa wakaguzi wa nje na ripoti zao ili kuzishughulikia na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza na kuiletea Taasisi hati chafu. Kamati hiyo pia inalo jukumu la kupitia taarifa ya fedha ya mwaka ya uhasibu kabla ya kusainiwa na Afisa masuhuli ili kuona kama kuna masuala yoyote yanayohitaji utatuzi na kuyatolea ushauri kabla ya kwenda nje ya Taasisi.

Mtendaji Mkuu aliongeza kuwa majukumu mengine ni kumshauri Afisa masuhuli wa Mahakama juu ya hatua za kuchukua kwenye masuala yanayohitaji uamuzi kulingana na taarifa za ukaguzi wa ndani na ule wa nje na taarifa za uwazi katika utawala, usimamizi wa fedha, mifumo ya udhibiti wa ndani ya Taasisi, mienendo ya kisheria, maadili ya usimamizi na wafanyakazi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania Bw. Pius Maneno wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo ulifanyika Mahakama ya Rufani Jijini Dar es salaam leo. 

Mwenyekiti mpya wa kamati ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania Bw. Pius Maneno akimkabidhi vitendea kazi Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Charles Magesa ambaye ni Mjumbe Mpya wa kamati hiyo.     

Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania Bw. Pius Maneno akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo uliofanyika Mahakama ya Rufani Jijini Dar es salaam . 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati mpya ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania mara baada ya uzinduzi wa kamati hiyo uliofanyika Mahakama ya Rufani Jijini Dar es salaam, kushoto kwake walioketi ni Mwenyekiti wa Kamati Bw. Pius Maneno na kulia ni Katibu wa Kamati Bw. Bwai Biseko.  

Wajumbe wa kamati mpya ya Ukaguzi ya Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa kamati hiyo uliofanyika Mahakama ya Rufani Jijini Dar es salaam.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni