Jumanne, 29 Septemba 2020

MWILI WA JAJI MMILLA WAZIKWA NYUMBANI KWAKE GOBA DAR ES SALAAM

Na Lydia Churi-Mahakama

Mwili wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Bethuel Mmilla umezikwa nyumbani kwake Goba Michungwani jijini Dar es salaam.

Mazishi hayo yalitanguliwa na Ibada iliyofanyika katika kanisa la Kiiinjili la Kilutheri Tanzania-K.K.K.T Usharika wa Mwenge jijini Dar es salaam kuanzia saa 6:00 mchana iliyoongozwa na Mchungaji Jacob Mwangomola.

Aidha, ibada hiyo ilihudhuriwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, wadau wa Mahakama na watumishi mbalimbali.

Akitoa salaam kwa niaba ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija limuelezea Marehemu Jaji Mmilla kuwa alikuwa ni kiongozi mwenye ushirikiano mkuwa na wenzake na aliyekuwa akiwatia moyo katika kazi mbalimbali za utoaji haki.

Naye Mwenyekiti wa chama cha wanasheria Tanzania (Tanganyika Law Society) Mhe. Dkt. Rugemeleza Nshalla amewashauri Majaji na Mahakimu kuandika hukumu zenye mguso chanya katika maisha ya watu na utawala wa sheria.

“Marehemu Jaji Mmilla aliandika hukumu nyingi ambazo zitatumika kama rejea kwa wanafunzi wanaosoma sheria nchini, Mahakimu pamoja na Majaji” alisema Jaji Mkuu.

Dkt. Nshalla pia aliwaasa familia ya marehemu kwa kuwataka waishi kwa kupendana na kushirikiana ili kuyaenzi mazuri aliyoyafanya.

Jaji Mmilla alifariki dunia usiku wa Septemba 25, 2020 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Awali marehemu alilazwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es salaam Septemba 23, 2020 alipokuwa akipatiwa matibabu na baadaye kuhamishiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alipofariki dunia.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongoza Wahe. Majaji  kutoa Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Bethuel Mmilla nje ya kanisa baada ya kumalizika kwa Ibada katika kanisa la K.K.K.T Usharika wa Mwenge jijini Dar es salaam. 


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongoza akiwa katika Ibada ya Mazishi ya aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Bethuel Mmilla. Kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Augustine Mwarija. 




Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na Mchungaji Jacob Mwangomola wakati wa Ibada ya Mazishi. 
Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Bethuel Mmilla likitolewa Kanisani mara baada ya Ibada ili kupelekwa makaburi Goba Michungwani jijini Dar es salaam.

 

Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Bethuel Mmilla likiingizwa kwenye gari tayari kwa kuelekea makaburini kwa Mazishi. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni