Jumatatu, 28 Septemba 2020

MWILI WA JAJI BETHUEL MMILLA WAAGWA KARIMJEE-DAR ES SALAAM

Na Mary Gwera, Mahakama

Mwili wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania (T), Marehemu Bethuel Mmilla umeagwa leo katika viwanja vya Karimjee vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla ya kuaga mwili wa marehemu Jaji Mmilla aliyefariki usiku wa Septemba 24, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema marehemu atakumbukwa kwa utendaji kazi wa kujitoa na ushirikiano.

“Wasifu wa Bethuel Mpakani Kasefu Mmilla ni mfano mzuri sana wa namna alivyowatumikia zaidi walio wengi kuliko alivyojitumikia kwa maslahi yake binafsi au maslahi ya familia yake. Wasifu wake unaonyesha kuwa kila kituo katika utumishi wake wa Mahakama, amekuwa ni wa kutumikia, anayetoa, na asiye wa kutumikiwa,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kuwa Maamuzi yaliyotolewa na marehemu Jaji Mmilla yatabaki kuwa mifano hai ya mambo yote aliyoyaamini na kuyatekeleza kwa vitendo.

Mhe. Jaji Prof. Juma aliongeza kuwa Jaji Mmilla atakumbukwa pia kwa ucheshi na utani wake wa mara kwa mara ambao uliwasaidia waheshimiwa Majaji wa Rufaa kusahau angalau kidogo, maswala magumu ya kisheria na kimaamuzi.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Mkuu amewashukuru madaktari, wahudumu wote wa Hospitali ya Jeshi Lugalo, Hospitali ya Taifa Muhimbili na wale wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiongozwa na Prof. Mohamed Janabi kwa kuwa karibu na marehemu.


Pichani ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiaga mwili wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, marehemu Bethuel Mmilla, hafla ya kuaga imefanyika mapema Septemba 28, Karimjee-Dar es Salaam.

Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Jaji Mmilla, nyuma ni baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani nao wakisubiri kutoa heshima za mwisho.
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani wakitoa heshima ya mwisho kwa mpendwa wao.
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiaga mwili wa marehemu Jaji Mmilla.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Jaji Kaijage na baadhi ya Majaji Wastaafu wa Mahakama ya Rufani wakitoa heshima za mwisho.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mmilla.

Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman (kulia) akiwa pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria katika hafla ya kuaga mwili wa marehemu Jaji Mmilla.
Mjane wa marehemu Jaji Mmilla (wa tatu kushoto mstari wa kwanza) akiwa pamoja na watoto wa marehemu na baadhi ya ndugu na jamaa mbalimbali walioshiriki katika hafla ya kuaga mwili Karimjee Dar es Salaam.
Pichani ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Jaji Semistocles Kaijage, Makamanda Wakuu wa Jeshi la Polisi nchini na wageni wengineo wakiwa katika hafla hiyo.
Baadhi ya Majaji Wastaafu wa Mahakama ya Tanzania, Watumishi na Wadau wengine wa Mahakama walioshiriki katika tukio hilo.

Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akitoa utaratibu wa tukio hilo.
Baadhi ya Naibu Wasajili wa Mahakama pamoja na Maafisa wengine wa Mahakama wakifuatilia kinachojiri katika tukio hilo.
Mjane wa Marehemu Jaji Mmilla, Bi. Flora Kissaka Mmila akiaga mwili wa mumewe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi akitoa heshima za mwisho.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha akiaga mwili wa marehemu Jaji Mmilla.
Watumishi wa Mahakama wakiaga mwili wa aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, marehemu Jaji Mmilla.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni