Na Paul
Mushi, Mahakama Kuu- Moshi
Mahakama Kuu Kanda ya Moshi imefanya Mafunzo maalum kwa jumla ya Mahakimu 21 wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya sita juu ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi.
Lengo la Mafunzo hayo ni kuwawezesha Mahakimu wote wa wilaya kanda ya Moshi juu ya kanuni, sheria na Maadili ya kushughulikia Mashauri ya Uchaguzi katika Kipindi hichi ambapo Tanzania inafanya uchaguzi Mkuu 2020.
Akifungua Mafunzo hayo hivi karibuni, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi-Mhe. Jaji Beatrice Mutungi amewasihi washiriki kusikiliza mashauri kwa uwazi, uhuru ili kuonyesha uhuru wa muhimili wa Mahakama hali itakayoongeza imani ya wananchi kwa Mahakama.
“Ninawasihi kufanya maamuzi kwa kuzingatia kanuni na sheria za nchi na kuepuka vishawishi vya rushwa pamoja na kusimamia maadili ya uhakimu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati,” alisema Mhe. Jaji Mutungi.
Naye Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Mhe. Bernazitha Maziku aliwataka washiriki hao kusikiliza kwa makini mada zitakazofundishwa ili ziwasaidie kuepuka migogoro itakayoweza kusababishwa kwa kukiukwa kwa taratibu za uendeshaji mashauri ya uchaguzi.
Mpaka sasa Mahakama kwa
kushirikiana na Chuo tayari imeshafanya mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya
uchaguzi kwa Maafisa mbalimbali wa Mahakama ikiwemo Majaji wa Mahakama ya
Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar, Naibu Wasajili,
Mahakimu Wakazi Wafawidhi lengo likiwa ni kuwawezesha kuyashughulikia kwa
ustadi zaidi na kwa wakati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni