Na Stanslaus Makendi, Mahakama Kuu Dodoma
Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania wametembelea na kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama iliyoko jijini Dodoma.
Majaji hao wakiambatana na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania
Mhe. Mohamed Chande Othman pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama ya Tanzania
walipata fursa ya kukagua miradi ya ujenzi inayoendelea kutekelezwa mkoani humo ikiwemo ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, jengo la Mahakama
Jumuishi “Intergrated Justice Centre”, pamoja na majengo ya Mahakama za Wilaya za Chemba na Kondoa ambayo baadhi imekamilika na tayari huduma za Mahakama zinatolewa
katika jengo hilo.
Jengo la Mahakama ya wilaya ya Kondoa lilikamilika na kuzinduliwa rasmi Februari 4 mwaka huu na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai na tayari linatumika kutoa huduma kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Viongozi hao, licha ya kukagua miradi ya ujenzi pia wametoa wito kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi mingine ya Mahakama nchini kuzingatia maelekezo ya kitaalamu, viwango vya ubora na kuhakikisha miradi hiyo inaendana na thamani ya fedha zilizoelekezwa katika miradi husika kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanachagiza maendeleo ya Taifa letu.
Sambamba na hilo, Viongozi hao wamepongeza Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa Mipango iliyowekwa inayolenga kuboresha miundombinu iliyopo na ujenzi wa majengo ya kisasa katika maeneo mbalimbali nchini ili kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi.
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Majengo cha Mahakama ya Tanzania, Mhandisi Khamadu Kitunzi akielezea jambo kwa Waheshimiwa Majaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni