Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemuapisha rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyeshinda kiti
cha Urais baada ya kutangazwa mshindi kufuatia kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa
Taifa uliofanyika Oktoba 28, 2020.
Sambasamba
na hilo katika hafla hiyo ya Uapisho wa Mhe. Rais wa awamu ya tano (5)
anayetumikia nafasi hiyo kwa muhula wa pili, Mhe. Jaji Mkuu alimuapisha pia
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma mapema Novemba 05, mwaka huu.
Akizungumza
na wananchi mara baada ya kuapishwa rasmi, Rais Magufuli aliwashukuru Watanzania
kwa kumpatia kura nyingi za ushindi na kuwaahidi kushirikiana nao katika
kuleta maendeleo ya Taifa.
“Uchaguzi
umekwisha, sasa tuchape kazi, napenda kuwahakikishia kama ilivyokuwa kwenye
miaka mitano iliyopita na kwa miaka mitano ijayo nitaendeleza na kutimiza yale
yote niliyoahidi,” alisema Rais Dkt. Magufuli.
Mhe.
Rais aliongeza kuwa ataendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali zilizopo nchini
ili ziendelee kutoa ajira, kuongeza fursa za uwekezaji na kutatua kero
mbalimbali.
Katika
hatua nyingine Mhe. Rais amesema Serikali itaendelea na mapambano dhidi ya
rushwa na ubadhilifu wa mali za umma, kukamilisha miradi mikubwa iliyoanza na
kutekeleza mingine mipya.
Kwa
upande wake, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Museveni aliyehudhuria
katika hafla hiyo amempongeza Mhe. Rais kwa ushindi aliopata na kuwapongeza
Watanzania kwa uchaguzi wa amani na wa kidemokrasia na kuwataka kuendeleza
uzalendo aliouacha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Hafla hiyo muhimu kwa Taifa ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongozana na Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Job Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Adelardus Kilangi, baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu pamoja na Viongozi wa Dini wakielekea katika nafasi zao kabla ya kumuapisha rasmi Mhe. Rais Magufuli.
Baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Tanzania pamoja na baadhi ya Viongozi na wageni wengine waalikwa wakiwa katika hafla hiyo.
Baadhi ya makundi ya Jeshi la Ulinzi na Usalama wakipita mbele ya Mhe. Rais.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni