Na Lydia Churi- Mahakama, Geita
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt.
Eliezer Feleshi amewataka watumishi wa Mahakama kusimamia maadili
wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku ili kutoa huduma bora kwa wananchi na
kulinda heshima ya Mhimili huo.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti na Watumishi wa Mahakama za wilaya za Bukombe na Chato
mkoani Geita, Jaji Kiongozi pia amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa
kushirikiana na kupendana wao kwa wao na wadau wote wa Mahakama wakiwemo
wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki zao.
“Simamieni
maadili ya kazi zenu, tuwe na ushirikiano mwema sisi wenyewe Pamoja na wadau wa
Mahakama”, alisistiza Jaji Kiongozi.
Katika
kuboresha utendaji kazi, Jaji Kiongozi aliwashauri watumishi wa Mahakama
kujiendeleza kielimu ili wawe na uwezo wa kufanya kazi Zaidi ya moja. Aidha,
aliwataka watumishi hao kujifunza na kuifahamu vizuri Taasisi wanayofanyia
kazi.
Watumishi
wapatiwe mafunzo/ ujuzi mbalimbali ili kuwawezesha kutekeleza vema majukumu yao
ya kila siku. Alisema watumishi wa kada za chini mara nyingi wamekuwa
wakisahaulika kupatiwa mafunzo hivyo ameutaka uongozi wa Mahakama kuhakikisha
watumishi hao pia wanapatiwa mafunzo ya kuboresha utendaji kazi wao.
Kuhusu
usikilizwaji wa mashauri, Dkt. Feleshi amewataka Majaji na Mahakimu kusikiliza
mashauri kwa haraka na ikiwezekana wasikilize hata siku ya Jumamosi ili kuondoa
msongamano wa mashauri mahakamani. Alisema mashauri yanayopaswa kupewa
kipaumbele ni yale ambayo watuhumiwa wake hawana dhamana ili kuondoa msongamano
magerezani.
Jaji
Kiongozi amewasisitiza Mahakimu kuhakikisha wanamaliza kwa haraka mashauri hususan ya Mirathi na yale ya Ndoa.
“Mashauri ya Ndoa yana athari kubwa kwa familia hasa Watoto, lakini pia
mashauri ya Mirathi nayo yanaathiri Watoto yatima, Wajane na Wagane hivyo
hayana budi kumalizika kwa wakati”, alisisitiza Jaji Kiongozi.
Akizungumza
katika ofisi za wakuu wa wilaya za Bukombe na Chato, Jaji Kiongozi amelishauri jeshi la polisi kuharakisha
kufanya upepelezi ili mashauri yamalizike kwa wakati.
“Polisi
harakisheni upelelezi, yapo mashauri yanayosubiri polisi kumaliza upelelezi na
Mkurugenzi wa Mashtaka kutoa vibali”, alisema Dkt. Feleshi.
Alisema
Mahakama imejiwekea mikakati ya kumaliza mashauri kwa wakati ikiwemo Majaji na
Mahakimu kupangiwa idadi ya mashauri wanayopaswa kumaliza katika kipindi cha
mwaka moja. Majaji wanatakiwa kusikiliza mashauri 220 na Mahakimu mashauri 250.
Jaji
Kiongozi amemaliza ziara yake ya siku tano ya kikazi katika Kanda ya Mwanza
ambapo alikagua shughuli za utendaji kazi katika Mahakama za wilaya za
Nyamagana, Ilemela, Misungwi, Kwimba, Magu, Ukerewe na Sengerema. Jaji Kiongozi
pia alitembelea Mahakama za wilaya za Bukombe, Chato Geita pamoja na Mahakama
ya Hakimu Mkazi Geita.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni