Na Francisca Swai- Mahakama Kuu Musoma
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. John Rugalema
Kahyoza amewataka Mahakimu wote walioko katika Kanda ya Musoma kutumia taaluma
yao kujibidisha kusoma sheria na kuzitafsiri kwa umakini.
Akifungua
mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri katika Mahakama za Mwanzo kwa
Mahakimu 36 wa Kanda hiyo, Mhe. Jaji Kahyoza alisema kuwa lengo la mafunzo hayo
ni kutatua changamoto zilizojitokeza wakati alipofanya ukaguzi wa robo ya tatu ya
mwaka 2020 katika baadhi ya Mahakama za Mwanzo zilizopo kwenye kanda ya Musoma.
Aidha,
Mafunzo hayo yalijikita katika taratibu za uendeshaji wa mashauri ya mirathi,
mashauri ya madai, mashauri ya jinai, uandishi wa hukumu kwa Mahakama za Mwanzo
na za Wilaya pamoja na utekelezaji wa hukumu.
Katika
mashauri ya mirathi, Mhe. Jaji Kahyoza kwa kushirikiana na Mkaguzi wa Ndani wa
Mahakama Kuu kanda ya Musoma Bw. Andala Odock, waliwasisitiza Mahakimu hao kuzingatia
taratibu zote za msingi tangu kupokelewa kwa shauri la mirathi hadi kufungwa,
zikiwepo taratibu za kuthibitisha msimamizi wa mirathi, namna ya kutunza wosia,
kuzingatia mgawanyo wa mali kwa warithi, mchakato wa malipo, na kufunga
mirathi.
Jaji
Kahyoza aliwasisitiza Mahakimu hao umuhimu wa kufungua mashauri ya mirathi pale
taratibu zote zinapokamilika pia mashauri hayo yafunguliwe eneo analotoka
marehemu kuepusha ufunguaji wa shauri moja mara mbili.
Kwa
upande wa mashauri ya madai na jinai, Mhe, Kahyoza, aliwataka Mahakimu hao kuzingatia
sheria na kuwa makini katika kurekodi ushahidi unaotolewa mahakamani na hatua
zote muhimu hadi kufikia wakati wa kutoa hukumu. Pia aliwakumbusha taratibu za
ukamataji mali wakati wa kukaza hukumu.
Naye
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma, Mhe. Zephrine Galeba, alimpongeza Jaji Mfawidhi kwa
kuandaa mafunzo hayo elekezi ya kujengeana uwezo na kukubali yafanyike kila
robo mwaka kwani yatasaidia sana kuboresha utendaji kazi hasa kwa Mahakimu wa
Mahakama za Mwanzo ambao huko ndiko mashauri mengi yanaanzia.
Jaji
Galeba pia aliwataka washiriki wote kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya
kazi pamoja na sheria ili kutoa maamuzi kwa uhuru jambo ambalo litalinda uhuru
wa Mahakama.
Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Sirari Mhe. Amina Ibrahimu Pessa akiwasilisha mada
ya Mirathi katika mafunzo hayo. Mbele ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ta Tanzania kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza akifuatilia Mada hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa kanda hiyo mara baada ya kufungua mafunzo yao kuhusu namna bora ya Uendeshaji wa Mashauri kwa Mahakama za Mwanzo. Wa pili kushoto ni Jaji wa Kanda hiyo Mhe. Zephrine Galeba. Kushoto ni Mtendaji wa
Mahakama kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya. Wengine ni Naibu Wasajili wa kanda hiyo, Mhe. Mary Moyo (wa pili kulia) na Mhe. Eugenia Rujwahuka (kulia).
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Ngoreme iliyoko wilayani Serengeti, Mhe. Adamu Peter Malima akichangia jambo wakati wa mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni