Na Festo Sanga, Mahakama Kuu-Kigoma
Mahakama ya Tanzania imewapatia Mahakimu Kanda ya Kigoma kompyuta mpakato (Laptop) ikiwa ni utekelezaji wa maboresho yanayoendelea ndani ya Mhimili huo yenye lengo la kuongeza matumizi ya vifaa vya TEHAMA kuchochea kasi ya utendaji kazi ili kutoa haki kwa wakati.
Akizungumza katika zoezi la ugawaji wa Kompyuta hizo mwishoni mwa wiki iliyopita, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Ilvin Mugeta aliwataka Wahe. Mahakimu kuhakikisha kompyuta walizopewa zinatunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kurahisisha jukumu kubwa la utoaji wa haki kwa wakati.
“Zama za Mali ya Umma haina uchungu zimepitwa na wakati hivyo kila mmoja atunze vifaa hivyo na kutumia ilivyokusudiwa” alisisitiza Jaji Mugeta.
Mhe. Jaji Mugeta alisema kuwa vifaa hivyo muhimu vitarahisisha utekekezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Jaji Mkuu kuhusu utoaji wa hukumu na mienendo ya mashauri katika kipindi cha siku 21 hadi 30. Aliongeza kuwa vifaa walivyovipata vina makusudi ya kufanya watimize jukumu kubwa na la misingi katika kuhakikisha mwananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.
Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma imepata jumla ya kompyuta thelathini mpakato (30), printer moja (1) na ‘Scanner’ tano (5) ambapo Vifaa hivyo vimegawiwa kwa walengwa katika tukio lililofanyika mapema Disemba 11, 2020. Mbali na Kigoma, Mahakama ya Tanzania imegawa.
Mbali na Kigoma Mahakama imegawa vitendea kazi hivyo kwa Majaji, Wasajili na Wasaidizi wa Sheria katika mikoa yote nchini ili kuwezesha kuchapa mienendo ya shauri, hukumu, amri na kadhalika na hatimaye kuwezesha upatikanaji wa nyaraka hizo kwa wakati.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Ilvin Mugeta (kushoto) pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Kigoma Bw. Moses Mashaka wakikagua moja ya Kompyuta zilizopokelewa mapema Disemba 11, 2020.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki akipokea kompyuta kutoka kwa Mhe. Jaji Mfawidhi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigoma, Mhe. Keneth Mugisha Mutembei(kushoto) akipokea Laptop kwa niaba ya Mahakimu wa wilaya ya Kigoma na Mahakama zote za Mwanzo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Ilvin Mugeta (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi wakiwa katika nyuso za furaha mara baada ya kupokea kompyuta mpakato (Laptop). Kutoka kushoto ni Mhe. Keneth Mutembei-Mahakama ya Wilaya Kigoma, wa pili kushoto ni Mhe. Fadhili Mbelwa -Mahakama ya Wilaya Kibondo, wa kwanza kulia ni Mhe. Gadiel Mariki-Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, na wa pili kulia ni Mhe. Iman Batenzi- Mahakama ya Wilaya Kasulu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni