Jumatano, 6 Januari 2021

MAKAMU WA RAIS KUFUNGUA MKUTANO MKUU WA TAWJA KESHO

            CHAMA CHA MAJAJI NA MAHAKIMU WANAWAKE (TAWJA)


                                            TAARIFA KWA UMMA

Mwanza- 06/01/2021

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) utakaofanyika Januari 7 hadi 9, 2021 katika ukumbi wa Benki Kuu (BOT) jijini Mwanza.

Mkutano huo utahudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ambao ni walezi wa chama hicho.

Viongozi wengine wanaotarajiwa kuhudhuria Mkutano huo ni pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika Mhe. Sylvain Or’e, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mwigulu Nchemba, pamoja na Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Geofrey Pinda.

Mkutano wa TAWJA utawakutanisha wanachama wake zaidi ya 200 wakiwemo Waheshimiwa Majaji, wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Wasajili, Naibu Wasajili, Mahakimu na Maafisa wengine wa Mahakama katika ngazi mbalimbali.

Ajenda ya mkutano kwa mwaka huu ni Uweledi na Ustawi wa Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania ‘Professionalism and welfare for women judges and magistrates in Tanzania catalyst for Change’. Aidha, katika mkutano huo pia mada mbalimbali za kujengeana uwezo zitatolewa kwa washiriki.

Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake hufanya Mkutano Mkuu kila baada ya miaka miwili kwa lengo la kutathmini shughuli mbalimbali zinazofanywa na chama na pia kuwajengea uwezo wanachama wake.

 

Imetolewa na

Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA)

  

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni