· Atoa Wito kwa Serikali Kusaidia kuwaelimisha wananchi kuhusu Mirathi
Na Lydia Churi-
Mahakama
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert
Chuma ametoa wito kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuisaidia Mahakama kuwaelimisha
wananchi wenye mashauri ya mirathi kufuata taratibu ili mashauri yao yamalizike
kwa wakati.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania alipofanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama katika mikoa ya
Njombe na Iringa kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili
wananchi pamoja na watumishi wa Mahakama kwenye maeneo hayo.
Akiwa mkoani Njombe, Mhe Chuma alipata wasaa wa
kukutana na viongozi wa Mkoa huo wakiwemo Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa
wilaya ya Wanging’ombe ambapo alitumia wakati huo kuwaomba viongozi hao
kusaidia kuwaelimisha wananchi taratibu mbalimbali za Mahakama na hasa
zinazohusiana na mashauri ya mirathi.
Alisema mashauri ya mirathi ni tatizo kwa nchi nzima na
kuwa tatizo hili linatokana na wananchi pamoja na Wasimamizi wa mirathi
kutokuwa na uelewa wa masuala ya Sheria kuhusu mirathi. Alitoa wito kwa
viongozi hao kutumia majukwaa yao kuwaelimisha wananchi na kuwahimiza wasimamizi
wa mirathi kukusanya mali na madeni ya marehemu, kisha kugawa na kufunga
mashaururi hayo kwa wakati.
Katika kuhakikisha tatizo la kutofungwa kwa wakati kwa
mashauri ya mirathi linamalizika, Msajili Mkuu amewaelekeza Mahakimu hasa wale
wa Mahakama za Mwanzo kusikiliza na kufunga mashauri hayo kwa mujibu wa sheria.
Amewataka pia Mahakimu hao kuandika vizuri mienendo ya mashauri hususani amri
zinazowaelekeza wasimamizi wa mirathi tarehe ya kufika mahakamani kwa ajili ya
kuwasilisha taarifa za mirathi na hatimaye kufunga mirathi.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Njombe, Mahakama za wilaya za Njombe na Wanging’ombe pamoja na Mahakama za
Mwanzo za Wanging’ombe na Njombe mjini, Msajili Mkuu aliwataka Watumishi hao
kuimarisha nidhamu na maadili na kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia Sheria
na taratibu katika kuwahudumia wananchi.
Aliwashauri watumishi hao kujiendeleza kitaaluma na
kujibidisha ili kuhakikisha wanapata elimu kuhusiana na masuala ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha utendaji kazi. Mhe. Chuma pia
aliwahimiza Mahakimu kuzitumia Kompyuta Mpakato walizopatiwa kwa mujibu wa
maelekezo yaliyotolewa. Ili kuhakikisha mashauri yanasikilizwa na kumalizika
kwa wakati, hivi karibuni Mahakama ya Tanzania iligawa kompyuta Mpakato
(Laptops) kwa Mahakimu wote nchini ili kuhakikisha lengo hilo linatimia.
Watumishi wa Mahakama pia walitakiwa kujiimarisha
katika matumizi ya mifumo mbalimbali iliyoanzishwa na Mahakama ili kurahisisha kutekelezaji
wa jukumu lake ka msingi la utoaji wa haki. Baadhi ya mifumo hiyo ya Mahakama ni
pamoja na mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri (JSDS ll) na ile ya TANZLII
pamoja na Tovuti ya Mahakama.
Kuhusu ushirikiano na Serikali pamoja na wadau wengine
wa Mahakama, Msajili Mkuu alisema mihimili yote ya Dola ina lengo moja la
kuwahudumia wananchi hivyo Mahakama iko tayari kushirikiana kwa kuwa mihimili
hii yote inategemeana ingawa kila moja uko huru na una mipaka yake.
Aliwakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutekeleza
jukumu lao la kusikiliza mashauri ya kinidhamu dhidi ya Mahakimu kwa mujibu wa
taratibu kwa kuwa wao ni wenyeviti wa kamati za maadili ya Mahakimu ngazi ya
Mahakama za Hakimu Mkazi, wilaya na Mwanzo.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania alifanya ziara ya
siku tatu Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa ambapo alikagua shughuli za
Mahakama katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mahakama za wilaya za Njombe
na Wanging’ombe pamoja na Mahakama za Mwanzo za Wanging’ombe na Njombe Mjini
kuanzia Desemba 28 hadi 30, 2020.
Ziara hiyo ilimuwezesha Msajili Mkuu wa Mahakama kukagua
shughuli za utoaji haki, kuzungumza na watumishi, kupokea taarifa za utendaji
kazi na kutoa maekekezo mbalimbali ya namna bora ya utatuzi wa changamoto alizobaini
wakati wa ziara hiyo.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe akiwa katika ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama.
Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe wakimsikiliza Msajili Mkuu wa Mwsajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akifanya ukaguzi wa shughuli za Mahakama katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni