Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (mwenye jaketi jeupe) akiwa kwenye Matembezi ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania leo jijini Dodoma ambapo alikuwa ni mgeni rasmi. Wa pili kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameushauri Mhimili wa Mahakama nchini kutumia Mitandao ya simu kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kupitia jumbe fupifupi.
Akifungua rasmi Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania mapema leo jijini Dodoma, Makamu wa Rais amesema kuwa kwa kufanya hivyo wananchi wengi watapata ufahamu juu ya taratibu mbalimbali za kimahakama.
“Hivi sasa mitandao ya simu imekuwa na desturi ya kutuma meseji mbalimbali kuhusu huduma kadhaa inazotoa, hivyo tumieni pia fursa hiyo pia kutumia mitandao ya simu kutoa elimu kuhusu taratibu za Mahakama ili wananchi wapate uelewa,” alisema Makamu wa Rais.
Akizungumzia matumizi ya lugha ya Kiswahili, Mhe. Suluhu ameiomba Mahakama kutumia Kiswahili hata katika machapisho yake kueleza taratibu mbalimbali za mhimili huo ili wananchi waweze kuelewa.
“Haitopendeza kuona Taifa huru ambalo Mahakama Kuu inatimiza miaka 100 bado wananchi wake walio wengi wanakosa haki zao za msingi kutokana na changamoto ya lugha Mahakamani,” alieleza.
Aidha, Makamu huyo wa Rais alitoa rai kwa Mahakama kuhakikisha kuwa katika mikakati yake ihakikishe kuwa sheria za nchi zinakuwa na tafsiri sahihi na malengo na azma ya kutungwa kwao na kuwa.
Kwa upande mwingine, Makamu wa Rais aliipongeza Mahakama kwa kutimiza miaka 100 ya Mahakama Kuu nchini tangu kuanzishwa kwake huku akimsifu Mhe. Jaji Mkuu kwa mageuzi na marekebisho mbalimbali katika sekta ya sheria.
“Mhe. Jaji Mkuu nafahamu tangu uteuliwe umesukuma mageuzi na marekebisho mbalimbali ya sheria kwenye Mahakama ili kuweza kuufanya mhimili huu kwenda na wakati lakini pia kuhimili mabadiliko. Nakupongeza sana wewe binafsi na Mhimili wote wa Mahakama kwa kutimiza miaka 100 mkiwa mmeimarisha vyema utendaji wa chombo chenu,” alisisitiza Mhe. Suluhu.
Kwa ujumla Mhe. Makamu wa Rais alipongeza pia maboresho mbalimbali ya Mahakama yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika huku akiahidi ushirikiano kutoka Serikalini ili huduma ya utoaji haki iendelee kutenda haki.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania-Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wananchi kutumia tovuti ya Mahakama kupata taarifa zinazohusiana na Mahakama.
“Nitumie nafasi hii kuwakaribisha wananchi wote watembelee Tovuti za Mahakama na za wadau wa sekta ya Haki ili kupata taarifa muhimu kila siku, wakati wowote na watoe maoni na mapendekezo kila siku yenye lengo la kuboresha utoaji haki nchini,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi kutembelea maonesho hayo na kuongeza kuwa wasiridhike na maboresho yaliyopo bali waendelee kudai maboresho zaidi yanayolenga kuwawezesha kupata haki.
Akizungumzia matumizi ya Kiswahili Mahakamani, Mhe. Jaji Prof. Juma alisema jitihada za kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inatumika katika ngazi zote za Mahakama zilianza tangu wakati TELFORD PHILIP GEORGES alipokuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kati ya mwaka 1965 na 1971.
“Mahakama ya Tanzania imeanza matayarisho ya awali ili kumbukumbu za mashauri na hukumu za Mahakama katika ngazi za Mahakama za Wilaya, za Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ziweze kupatikana papo hapo, katika lugha ya Kiswahili na kwa lugha ya kiingereza kabla ya mwisho wa mwaka huu,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Katika hafla hiyo, Mhe. Suluhu alizindua pia miongozo mbalimbali ya Mahakama ikiwemo muongozo wa Dhamana, mwongozo wa utekelezaji wa mashauri, mwongozo wa usimamizi wa uondoshaji wa vielelezo, mwongozo wa madalalina Wasambaza nyaraka za Mahakama.
Mingine ni mwongozo wa watumiaji wa huduma za Mahakama, Mwongozo wa utoaji hukumu kwa Maofisa wa Mahakama na Mwongozi wa kushughulikia mashauri yanayohusu makundi maalum.
Maadhimisho ya wiki ya sheria yaliyozinduliwa rasmi leo na kilele cha Siku ya Sheria Nchini, huashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Kimahakama ambao ni mwanzo wa shughuli za Mahakama katika mwaka. Maonesho hayo ambayo yanafanyika kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ yameshirikisha wadau mbalimbali kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka na wengineo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni