· Jaji Mkuu atoa wito kwa wananchi kuitembelea Tovuti ya Mahakama
Na Lydia Churi- Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis ametoa wito kwa wananchi kujenga
mazoea ya kuitembelea Tovuti ya Mahakama ya Tanzania mara kwa mara ili wawe na uelewa
mpana wa masuala ya kisheria hasa wanapotaka kufungua mashauri mahakamani au
kukata rufaa.
Akizungumza
na Waandishi wa leo kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya
Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Mkuu amesema tovuti ya Mahakama imesheheni
taarifa muhimu ambazo wananchi wakizipata zitasaidia haki kupatikana kwa
urahisi.
“Nawaomba
Watanzania wakumbuke kuwa wanaweza kupata taarifa wakati wowote ule kuhusu
shughuli za Mahakama kwa kutembelea Tovuti ya Mahakama, wananchi wakiwa na
tabia ya kuelewa masuala hayo itasaidia upatikanaji wa haki kwa wakati”,
alisisitiza Jaji Mkuu.
Kwa
mujibu wa Prof. Juma, moja ya malengo matano ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2025, ni kuwepo kwa jamii
iliyoelimika na inayojifunza. Aliongeza kuwa taifa linalojifunza ni lile ambalo
wananchi wake, kwa juhudi zao, wanatafuta taarifa na elimu wao wenyewe bila kusubiri
vyombo vya habari.
Kuhusu
maadhimisho ya wiki ya Sheria, Jaji Mkuu alisema wiki hiyo itatanguliwa na matembezi
yatakayofanyika
tarehe 24/1/2021 yatakayoongozwa na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Alisema
matembezi hayo yataanzia Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma na kuishia
kwenye viwanja vya Nyerere ambapo yatawakutanisha pia wadau mbalimbali wa
Mahakama.
Alitoa
wito kwa wananchi wa Dodoma, maeneo ya jirani pamoja wananchi wote wa Tanzania wenye
malalamiko, maoni na mapendekezo ya uboreshaji wa huduma za Mahakama wafike
kwenye maonesho ya wiki ya sheria ili kupata ufumbuzi.
Alifafanua kuwa wananchi watakaotembelea
mabanda ya Mahakama watapata fursa ya kujifunza kwa kiasi gani Mahakama ya
Tanzania imejipanga kutoa haki katika Karne ya 21 kwa ufanisi kwa matumizi ya
TEHAMA.
Baadhi
ya mambo yatakayotolewa elimu ya Sheria ni pamoja na taratibu za ufuanguaji wa
mashauri, Sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, ndoa na talaka,
utekelezaji wa hukumu, Sheria za
Watoto na taratibu za mashauri ya mirathi.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, elimu itakayotolewa
pia itahusu msaada wa kisheria, ushughulikiwaji wa malalamiko mbalimbali na
kupokea maoni na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha shughuli za Mahakama na
sekta nzima ya sheria, mifumo ya TEHAMA katika uendeshaji wa mashauri na maboresho
ya Sheria na Kanuni.
Jaji Mkuu alisema kilele cha maadhimisho ya siku ya
Sheria nchini kitafanyika Februari 1, 2021 katika viwanja vya Chinangali jijini
Dodoma. Kauli mbiu ya wiki ya sheria ni “Miaka 100 ya Mahakama Kuu: Mchango
wa Mahakama katika Kujenga Nchi inayozingatia Uhuru, Haki, Udugu, Amani na
Ustawi wa wananchi 1920-2020”
Sambamba
na elimu ya sheria itakayotolewa kwenye Maonesho yatakayofanyika kitaifa mkoani
Dodoma kuanzia Januari 23 hadi 29, 2021, elimu ya sheria pia itatolewa katika
Kanda za Mahakama Kuu, Mikoa na Wilaya nchi nzima kama ilivyofanyika kwa miaka
mingine.
Katika maonesho hayo, elimu hiyo itatolewa na waheshimiwa
Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili, na Mahakimu pamoja na wadau wa Mahakama
wakiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya
Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi,
Magereza, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na wengine.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzani Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru (kulia) wakifuatilia jambo wakati wa Mkutano na Waandishi wa habari. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza wakati wa Mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni