· -Aisifu Mahakama kwa maboresho
· -Aiomba Mahakama kuandika andiko/kitabu cha historia ya Mahakama Kuu ilipotoka, ilipo na inapoelekea
Na Mary Gwera, Mahakama
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi ameisifu Mahakama ya Tanzania kwa hatua ya maboresho iliyopiga inapoadhimisha miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kukagua mabanda ya Mahakama na Wadau wa Mahakama walioshiriki katika Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania mapema Jan 29, 2021, Prof. Kabudi amesema kuwa kumekuwa na mabadiliko ya dhahiri ndani ya Mahakama ikiwemo miundombinu bora ya majengo yake, teknolojia na kadhalika.
“Nimekagua mabanda nimeona na kufurahishwa na jinsi Mahakama ilivyopiga hatua, ombi langu ni kuangalia jinsi ya kuandika kitabu kitakachoonyesha historia ya Mahakama Kuu katika kipindi cha miaka 100 ilipotoka, ilipo na inapoelekea,” alisema.
Kwa upande mwingine, Waziri Kabudi ameishauri Mahakama inapoendelea na safari ya matumizi ya TEHAMA isisahau pia kuweka kumbukumbu muhimu.
“Si kwamba nakataa matumizi ya teknolojia, bali natoa angalizo pia ya kuweka kumbukumbu na taarifa muhimu kama ‘backup’ kwa ajili ya rejea kwa vizazi vijavyo na kuweka historia nzuri kwa ajili ya Taasisi,” alisema Prof. Kabudi.
Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania yamehitishwa leo Januari 29, 2021 nchi nzima, huku kilele cha wiki hii kikitarajiwa kuwa Februari mosi mwaka huu, ambapo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Katika siku ya mwisho ya maonesho hayo, wageni mbalimbali wamepata fursa ya kutembelea katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma ikiwa ni pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Magoiga, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na wananchi wengine.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi
akiwa katika uso wa furaha wakati akiangalia miongoni mwa nyaraka za Mahakama
zilizokuwa zikitumika miaka ya nyuma. Katikati ni Naibu Msajili-Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. David Ngunyale na kulia ni Mkuu wa Maktaba-Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Hakimu, Mhe. Kifungo Mrisho.
Prof. Kabudi akipata maelezo kutoka kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Hussein Mushi (wa kwanza kulia) pindi alipotembelea banda la Kurugenzi ya Menejimenti ya Mashauri ya Mahakama ya Tanzania.
Akiendelea kupata maelezo kuhusiana na banda hilo.
Mhe. Waziri Kabudi alipata pia fursa ya kutembelea banda la Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Prof. Kabudi akifurahia baadhi ya picha zilizokuwa zikionekana katika bango. Katikati ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na kulia ni Bw. Humphrey Paya, Mtendaji- Mahakama za Mwanzo nchini.
Mhe. Kabudi akiwa katika banda la Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi akipata maelezo kuhusu Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kutoka kwa mmoja wa Maafisa kutoka chuo hicho.
Prof. Kabudi akiwa katika banda la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni