· Ampongeza Jaji Galebu kwa uandishi wa hukumu kwa Kiswahili, amteua kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani
· Apongeza maboresho ya Mahakama ndani ya miaka 100 ya Mahakama Kuu
Na Lydia Churi na Mary Gwera, Mahakama
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa rai kwa Mhimili wa Mahakama kuweka mkakati wa kutumia lugha ya Kiswahili Mahakamani kwa manufaa ya wananchi huku akimpongeza na kumteua Jaji Zephrine Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa kuonyesha uzalendo wa kuandika hukumu kwa kutumia Kiswahili.
Rais Magufuli ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma, alisema kuwa Kiswahili ni miongoni mwa lugha kubwa duniani, ambayo inatumiwa na Watanzania wengi.
“Nitumie fursa hii, kumpongeza sana Mheshimiwa Jaji Galeba wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kwa kutumia Kiswahili katika kutoa hukumu kwenye Kesi ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi katika kesi ya Mapitio Na. 23 ya Mwaka 2020. Huyu ni Mzalendo wa kweli wa lugha ya Kiswahili kwenye Mahakama. Na kwa sababu 27 ya uzalendo wake, kuanzia leo, namteua kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa,” alisema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais alisema kuwa kushindwa kuitumia Lugha hii kwenye masuala ya Kimahakama na Kisheria sio tu kunawanyima haki wananchi, bali pia kuwaongezea gharama kupitia ukalimani wa kutafsiri hukumu na mienendo ya kesi.
Aliendelea kwa kutoa rai kwa kuwasihi wadau wote wa Mahakama, ikiwemo Mahakama, Bunge, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuandaa Mkakati wa kuwezesha lugha ya Kiswahili kwenye masuala ya Sheria na Mahakama, ikiwemo kuendelea kuzitafsiri Sheria za zamani na kutunga Sheria mpya kwa lugha ya Kiswahili.
Kwa upande mwingine, Mhe. Rais alizungumzia pia tatizo la ucheleweshaji wa mashauri kuwa bado lipo, hususan mashauri yanayohusu masuala ya biashara na mikopo ambayo yanazorotesha ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Ipo tabia ya baadhi ya wateja wa Benki kukimbilia Mahakamani na kufungua kesi nyingi au kuweka mazuio kwa lengo la kuchelewesha urejeshaji wa mikopo wanaodaiwa na benki. Kesi za namna hiyo zipo nyingi, na nyingine zina zaidi ya miaka mitano hazijaamuliwa,” alieleza Mhe. Rais.
Alitoa mifano ya kesi zilizofunguliwa Mahakamani na wateja wakubwa wa Benki nne ambazo ni Benki ya Posta Tanzania (TPB), Benki ya Azania (Azania Bank Ltd) na Benki ya Maendeleo (TIB).
“Hali hii ya wadaiwa kukimbilia Mahakamani na kesi kuchelewa kutolewa maamuzi, imekuwa na athari nyingi za kiuchumi kwa nchi yetu. Baadhi ya athari hizo ni kupungua kwa uwezo wa benki zetu kutoa mikopo kwa wateja; (ii) kuongezeka kwa gharama za riba kutokana na benki kulazimika kuongeza riba na kadhalika,” alieleza.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa Desemba 31, 2020 inaonyesha kuwa Azania Bank Ltd ina kesi 36 zilifunguliwa na wadaiwa wake zenye thamani ya shilingi bilioni 352.27; Benki ya Maendeleo (TIB) ina kesi 44 zenye thamani ya shilingi bilioni 167.267; Benki ya TPB ina kesi 16 zilizofunguliwa na wadaiwa wake zenye thamani ya shilingi bilioni 6.2; CRDB ina kesi 282 zenye thamani ya shilingi bilioni 113.25.
Akizungumzia Maadili ya Watumishi wa Mahakama, Mhe. Rais alimpongeza Mhe. Jaji Mkuu kwa hatua kinidhamu zilizochukuliwa na Mahakama dhidi ya Maafisa wake wanaoichafua Taasisi huku akitoa wito kwa Kamati za maadili za Maafisa wa Mahakama za Mikoa na Wilaya kukutana.
“Hata hivyo, nimesikitika sana na taarifa kwamba, Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama za Mikoa na Wilaya, ambazo kisheria zinaongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya zimekuwa hazikutani; na hivyo, kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wenye makosa. Napenda kutumia fursa hii kuagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote kuhakikisha Kamati hizo za Maadili 24 zinakutana ili kujadili masuala ya maadili ya watumishi wa Mahakama. Naagiza pia Wakuu wote wa Mikoa kuwasilisha Ripoti vya Vikao vya Kamati hizo mwezi huu,” alisisitiza Mhe. Rais.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameiomba Serikali na Bunge kuyapa kipaumbele mahitaji ya Mahakama yaliyooneshwa katika mpango wa miaka mitano wa maendeleo ya miundombinu ya Mahakama 2016/17-2020/2021 itakapojadili na kupitisha Mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano.
“Mhimili wa Mahakama peke yake hauwezi kutatua changamoto bila kuwezeshwa na Mihimili ya Serikali na Bunge inayosimamia rasilimali za aina zote, hapa napenda kutambua namna mihimili ya Serikali na Bunge ilivyokubali jukumu la kutatua changamoto zinazoikabili Mahakama ya Tanzania”, alisema Jaji Mkuu.
Kwa mujibu wa Prof. Juma, mfano wa Mhimili wa Mahakama kuwezeshwa na Serikali ni kukamilishwa kwa mazungumzo na Benki ya Dunia kuhusu namna ya kusaidia kuendeleza juhudi za maboresho ya utoaji huduma za Mahakama kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za kuboresha shughuli na huduma za Mahakama.
Mwaka 2016, Benki ya Dunia iliridhia kuisaidia Mahakama ya Tanzania kupitia Serikali ya Tanzania kupata fedha za mkopo wenye masharti nafuu uliogharimu Dola za Marekani milioni 65 ambazo ni saw ana shilingi bilioni 139.5 za kitanzania.
Akizungumzia namna mhimili huo ulivyowezeshwa, Jaji Mkuu alisema miongoni mwa mafanikio yaliyotokana na uwezeshwaji huo ni kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu kanda za Kigoma na Musoma. Aliongeza kuwa, Mahakama inatarajia kukamilisha ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu nyingine sita katika miji ya Mwanza, Arusha, Dodoma, Morogoro pamoja na wilaya za Temeke na Kinondoni mkoani Dar es salaam.
Alisema katika kuendelea kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi, Mahakama ya Tanzania inatarajia kuanza ujenzi wa majengo ya Mahakama za wilaya 25 katika mwaka wa fedha 2020/21. Alisema ujenzi huo utawapunguzia mzigo wananchi ambao hulazimika kupata huduma kwenye Mahakama za wilaya jirani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza wakati wa sherehe ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma Februari 01, 2021.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akitoa hotuba yake kwa Viongozi na wananchi mbalimbali waliohudhuria katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania.
Baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania 1921-2021.
Baadhi ya Viongozi Serikali na wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama walioshiriki katika hafla hiyo.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama na wananchi mbalimbali walioshiriki katika Maadhimishisho ya siku ya sheria nchini.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikagua gwaride maalum kuashiria uzinduzi rasmi wa shughuli za Mahakama kwa mwaka 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni