Na Festo Sanga, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Ilvin Mugeta amefurahishwa na kupongeza jitihada za utendaji kazi bora wa Mahakama za Mwanzo katika Kanda hiyo kwa kutekeleza kwa vitendo mpango wa kanda unaohusu viwango vya muda maalum wa usikilizaji wa mashauri hali iliyopekelea mahakama hizo kuvuka miaka miwili mfululizo 2020 na 2021 kwa mashauri sifuri.
Pongezi hizo amezitoa kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya kikazi katika wilaya za Kigoma, Kasulu na Kibondo iliyoanza Machi 5, 2021 ambayo ilihusisha pia shughuli zingine za ukaguzi wa Mahakama ikiambatana na utoaji wa vyeti vya pongezi kwa watumishi wa Mahakama za mwanzo 19 zilizofanya vizuri.
“Natambua na kuheshimu mchango wa kila mtumishi alioutoa katika kuhakikisha mashauri yanamalizika kwa viwango vinavyokubalika katika kanda ndio maana nawapatia vyeti vya pongezi kwa kazi hiyo nzuri” alisema Jaji Mugeta.
Aliongeza kuwa Mahakama ngazi zote katika Kanda hiyo zimefanya vizuri katika kutekeleza mpango wa viwango vya muda wa usikilizaji mashauri lakini Mahakama za Mwanzo zimefanya vizuri zaidi licha ya changamoto za miundombinu ya utendaji kazi.
“Jumla ya mashauri 3,416 yalimalizika kwa kipindi cha mwaka 2020 katika Mahakama za Mwanzo huku Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Nguruka iliyopo Wilaya ya Kigoma Mheshimiwa William Mugisa Soga akiibuka kinara kwa kusikiliza na kuamua mashauri 428 akifuatiwa na Mheshimiwa Mbuke James Luchunga wa Mahakama ya Mwanzo Ujiji- Kigoma aliyesikiliza na kutolea uamuzi mashauri 422,” alieleza Mhe. Jaji Mugeta.
Wakati huohuo, Jaji Mfawidhi alisema mpango wa kanda wa kushindanisha watumishi utahamia kwenye ubora wa kazi pamoja na idadi ya mashauri yaliyomalizwa na Hakimu, pia ubora wa hukumu zilizotolewa na Hakimu zitaangaliwa katika kigezo cha ubora na kupata washindi wa Kanda ya Kigoma.
Aliongeza kuwa ni matarajio ya Kanda kuwa viwango vya ushindani vitakuwa vinabadilika kwa kadri vitakavyokuwa vinakubalika na kuwa anatarajia kuona ushindani huo ukiongeza chachu ya utendaji kazi ili kuleta tija na ufanisi.
“Majaji na Mahakimu tutakuwa katika kapu moja la ushindani, huku watumishi wasio Mahakimu wakipimwa kupitia mfumo wa wazi wa utendaji kazi (OPRAS) na zawadi zitatolewa siku ya Mei Mosi 2021” alisisitiza Jaji Mugeta.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Bw. Moses Mashaka alisema mpango na dhamira ya Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma ni kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi ya kufanyia kazi kwa kutekeleza mpango wa kanda wa kukarabati miundo mbinu ya majengo hususani Mahakama za mwanzo ili kuruhusu matumizi ya TEHAMA pamoja na kutoa motisha kwa watumishi wanaofanya vizuri katika utendaji kazi na eneo la maadili.
Hatua hiyo ya Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kutambua mchango na jitihada za watumishi katika utendaji kazi kutawaongezea ari na morali ya kufanya kazi na hatimaye kuvuka malengo ya utendaji kazi.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Kigoma akisalimiana na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu pindi alipowasili Wilayani hapo kwa ziara ya kikazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni