Jumatano, 10 Machi 2021

MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA KAZI YATOA MSAADA KWA WATOTO YATIMA

Na Innocent Kansha – Mahakama

Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi imetoa msaada wa vyakula na vifaa mbalimbali katika Kituo cha Watoto Yatima cha Almadina kilichopo Tandale kwa Tumbo kata ya mwananyamala Jijini Dar es Salaam ikiwa ni katika kusherehekea Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2021.

Akitoa msaada huo kwa niaba ya watumishi wa Mahakama hiyo, Afisa Utumishi Bi. Beatrice Dominic alisema wametoa msaada katika kituo hicho kwa mwaka wa pili mfululizo wakionyesha imani kubwa kwa kundi hilo lenye uhitaji maalumu.

“Ni mwaka wa pili sasa tunatoa msaada katika kituo hiki, hii inamaanisha kwamba Mahakama siyo kisiwa inashirikiana na jamii inayoiuzunguka,” alisema Bi. Beatrice.

Aidha, Afisa huyo aliorodhesha vitu vilivyotolewa watoto hao yatima kuwa ni mchele kilo 50, sabuni ya kufulia ndoo tatu (3), maharage kilo 10, mafuta ya kupikia lita 10, unga wa dona kilo 50, maziwa ya unga kilo nne (4), Sukari kilo 20, Majani ya chai kilo moja na nusu, Ngano kilo 25, miche ya sabuni 15, chumvi katoni moja, viberiti katoni moja kituo na nyama kilo 9.

Naye, Msimamizi wa kituo hicho Bi. Kulthum Yusuph alipongeza na kushukuru kwa msaada huo uliotolewa na Uongozi wa Mahakama kwa niaba ya walezi na watoto wa hicho.

“Sisi ni kituo tulichopendelewa kwa miaka miwili mfululizo msaada huu umetufikia utaongeza morali ya watoto kujituma katika masomo yao na kuwajengea imani kwa Taasisi ya Mahakama na kuwa mabalozi wazuri kwao na kwa jamii inayowazunguka”, alieleza Bi. Kulthum.

Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Bi. Beatrice Dominic (kulia) akimkabidhi msaada wa bidhaa mbalimbali Msimamizi wa Kituo cha kulea Watoto Yatima cha Almadina kilichopo Tandale kwa Tumbo kata ya Mwananyamala Jijini Dar es Salaam, Bi. Kulthum Yusuph, huku baadhi ya watoto hao wakishuhudia zoezi hilo.

Baadhi ya Watoto Yatima wa Kituo cha Almadina  wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kupokea msaada wa vitu mbalimbali kutoka Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi wakiwa katika picha ya pamoja na Watoto na Msimamizi wa kituo hicho mara baada ya zoezi la kukabidhi msaada wa vitu mbalimbali.

(Picha na Innocent Kansha – Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni