Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa Watumishi
wanawake wa Mahakama kusimama katika nafasi zao kama Viongozi ili kuhakikisha
usawa wa kijinsia unazingatiwa katika mfumo mzima wa utoaji haki nchini.
Akizungumza
na baadhi ya Watumishi wanawake wa Mahakama Machi 08, 2021 katika hafla fupi ya Maadhimisho ya
siku ya Wanawake Duniani iliyoandaliwa na Chama cha Majaji Wanawake Tanzania
(TAWJA), Mhe. Jaji Prof. Juma alisema kuwa kila mwanamke katika nafasi yake ni
Kiongozi.
“Kila Mwanamke ni kiongozi, kiongozi ni mtu
ambaye katika nafasi yake anayo nafasi ya maamuzi, hivyo maamuzi yenu yaonyeshe
njia kwa wengine kufuata: kila mmoja wenu hapa, na wenzenu katika nafasi mbali
mbali za Mahakama, ni viongozi,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Aidha,
Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa katika mapambano ya kutafuta usawa, safari iliyopo
mbele bado ni ndefu na ngumu kuliko mafanikio yanayoweza kuyaorodheshwa.
“TAWJA,
kama Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake ni kiongozi, na kipo katika mstari
wa mbele kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa katika mfumo mzima wa
utoaji haki nchini na kuwezesha wanawake kupewa fursa sawa katika nyanja zote
ili tuwe na Taifa ambalo ubaguzi na ukatili wa kijinsia haupewi nafasi yoyote,”
alisema Mhe. Jaji Mkuu.
Akirejea
Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kikao cha 65 cha Kamisheni ya
nafasi ya wanawake (COMMISSION ON THE STATUS OF WOMEN) kuhusu ushiriki kamilifu
wa wanawake katika kufikia maamuzi kuhusu masuala ya umma, na kuhimiza usawa wa
kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote itakayokutana Machi 15
hadi 16, 2021, Mhe. Jaji Mkuu amebaini ya kuwa safari bado ni ndefu hadi
kufikia Usawa wa Jinsia.
“Nitawaomba
muisome hiyo ripoti ili itusaidie kupanga mikakati ya safari hiyo ndefu iliyo
mbele yetu,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.
Aidha
Mhe. Jaji Mkuu aliainisha baadhi ya maeneo hayo ambayo ni Wanawake kuwa na uwakilishi
mdogo katika sehemu zote za utoaji maamuzi katika taasisi za umma na Ukatili
dhidi ya wanawake bado umeenea.
Aliongeza kuwa Wanawake wengi zaidi ya
wanaume, bado wanaishi kwenye umasikini mkubwa, na wanayo nafasi chache za
kupata mikopo, wanabeba mzigo mkubwa zaidi wa kutunza familia, na sheria na
taratibu za kisheria bado haziwapi nafasi sawa kupata haki na unafuu.
Mhe Jaji Mkuu alishauri kuwa ili wanawake waweze
kufikia daraja la usawa katika ushiriki na utoaji maamuzi katika maswala ya
umma, nchi lazima zikubali kwa dhati kutekeleza yale yote yaliyoahidiwa na nchi
katika Mikataba ya Haki za Binadamu na katika Sheria na Kanuni za nchi husika
ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira na mifumo ambayo itapunguza ukatili dhidi
ya wanawake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAWJA, Mhe.
Jaji Joaquine De Mello alisema anaishukuru Serikali pamoja na Mahakama kwa
jitihada za kuhakikisha kuwa Mwanamke anakuwa katika nafasi za maamuzi.
Akitoa
baadhi ya takwimu za uwiano wa Wanawake na wanaume, Mhe. Jaji De-Mello alisema
katika ngazi ya Mahakama ya Rufani kuwa jumla ya Majaji wanawake saba (7) kati ya Majaji wanaume nane
(8), Mahakama Kuu, Majaji Wanawake 23 kati ya wanaume 48, Mahakimu Wakazi
wanawake 486 kati ya wanaume 507.
“Safari
ya kuwa na usawa kati ya wanaume na wanawake bado ni ndefu, ila tunashukuru
Serikali na Mahakama kwa kuendeleza jitihada za kuhakikisha kuwa usawa
unafikiwa,” alisema Jaji De Mello.
Waheshimiwa
Majaji pamoja na baadhi ya watumishi wanawake wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika
hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni