Na Lydia Churi-Mahakama
Hivi karibuni Mahakama ya Tanzania pamoja na shirika
la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala
ya Miliki Bunifu (World Intellectual Property Organisation-WIPO) walisaini mkataba wa makubaliano (Memorundum of
Understanding) unaolenga kuendeleza ushirikiano katika kuimarisha huduma za
kimahakama.
Mkataba huo ulisainiwa Machi 5, mwaka huu kati ya
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma kwa upande wa Mahakama
ya Tanzania pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Miliki Bunifu (WIPO) Bw.
Daren Tang.
Baadhi ya maeneo yaliyokubaliwa katika ushirikiano huo
ni pamoja na kubadilishana uzoefu wa shughuli za Mahakama na kushirikiana
kujengeana uwezo katika kazi za Mahakama kupitia mikutano na semina kwa Majaji na
Mahakimu, uandaji wa majumuisho ya sheria na kesi zinazohusu miliki bunifu (Compendium
of IP laws and digest of cases)
Maeneo mengine ya ushirikiano huo ni pamoja na kubadilisha
taarifa zinazohusu maamuzi ya kimahakama, kushirikiana katika kufanya tafiti
zinazohusu masuala ya miliki bunifu, kushirikiana katika kusisitiza matumizi ya
njia ya usuluhishi katika utatuzi wa migogoro pamoja na maeneo mengine
yatakayokubaliwa na pande zote mbili.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano
hayo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania alisema kusainiwa kwa mkataba huo
kunarasimisha ushirikiano uliokuwepo kati ya Mahakama ya Tanzania na shirika la
WIPO.
Alisema mafunzo ya kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu
yaliyofanyika nchini Tanzania mwaka 2019 yamesaidia kuwaongezea ujuzi watumishi
hao wa Mahakama hivyo aliishukuru WIPO kushirikina na Mahakama ya Tanzania katika
kuandaa mafunzo hayo muhimu katika shughuli za utoaji haki nchini.
Msajili Mkuu pia aliwashukuru Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja
na Mwakilishi wa Tanzania katika shirika hilo Mhe. Upendo Ngitiri ambaye ni Hakimu
Mkazi- Kurugenzi ya Usimamizi wa
mashauri kwa jitihada zao zilizowezesha Mahakama ya Tanzania na WIPO kusaini mkataba
wa makubaliano hayo.
Akizungumza wakati wa utiaji Saini wa Mkataba huo,
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la WIPO Bw. Daren Tang aliipongeza Tanzania na
kueleza kuwa utafiti uliofanywa na
jarida la kimataifa linalopima nchi mbalimbali katika masuala ya
uvumbuzi (Global Innovation Index (GI)) katika
utafiti wake ilieleza kuwa mwaka jana Tanzania ilishika nafasi ya kwanza kati ya nchi 16 zenye kipato
cha chini (kwa wakati huo ) na nafasi ya nne (4) kati ya nchi 26 za
kusini mwa jangwa la Sahara.
Bw. Tang alizitaja sababu za Tanzania kufanya vizuri
kuwa ni uwepo wa miundonmbinu mizuri ya ubunifu, mazingira mazuri ya
kimawasiliano kati ya Tanzania na mataifa mengine na ongezeko la viwanda.
Hafla ya kusainiwa kwa mkataba huo ilifanyika kwa njia
ya mtandao na kuhudhuriwa na viongozi wa Mahakama ya Tanzania akiwemo Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe. Stephen Magoiga ambaye alitoa
ujumbe wa Mahakama kwa niaba ya Jaji Mkuu pamoja na viongozi wengine wa juu wa Mahakama.
Viongozi wa WIPO na Balozi wa Tanzania nchini Geneva Mhe. Maimuna Tarishi
aliyewakilisha Tanzania nchini humo pia walikuwepo kwenye half hiyo.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Miliki Bunifu (WIPO) Bw. Daren Tang wakisaini Mkataba wa Makubaliano (Memorundum of Understanding) kati ya Mahakama ya Tanzania na shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Miliki Bunifu (World Intellectual Property Organisation-WIPO) unaolenga kuendeleza ushirikiano katika kuimarisha huduma za kimahakama.
Hafla ya kusainiwa kwa Makubaliano hayo kama inavyoonekana katika picha.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara Mhe. Stephen Magoiga ambaye alitoa ujumbe wa Mahakama kwa niaba ya Jaji Mkuu akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Hafla ya kusainiwa kwa Makubaliano hayo kama inavyoonekana katika picha kwa upande wa Tanzania. Upande wa pili walisaini Mkataba huo nchini Geneva.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni