Na Lydia Churi-Mahakama, Njombe, Morogoro
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na
Sheria wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa matumizi mazuri ya rasilimali
yanayodhihirishwa na hali nzuri ya miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama
inayoendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Wajumbe wa kamati hiyo wametoa pongezi hizo wakati wa
ziara yao ya kukagua baadhi ya miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama katika
mikoa ya Dodoma, Njombe na Morogoro. Mkoani Dodoma, wajumbe hao walikagua
ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa, Mahakama ya Hakimu Mkazi
Njombe na jengo la Mahakama Kuu Jumuishi kanda ya Morogoro.
“Tunaipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kujenga majengo
mazuri katika maeneo mbalimbali nchini, majengo haya ni ya viwango vya nchi ya
uchumi wa kati” alisema Makamu Mwenyeikiti wa Kamati hiyo Mhe. Najma Murtaza
Giga.
Mhe. Giga alisema ubora wa majengo ya Mahakama
unatokana na maono ya mbeleni ambapo jengo la Mahakama ya Mwanzo
lililojengwa linaweza kutumika kutoa
huduma za Mahakama ya wilaya pindi eneo husika linapopanda hadhi na kuwa wilaya
huku akitolea mfano jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa lililopo kwenye wilaya
ya Kongwa mkoani Dodoma.
Mjumbe mwingine wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Singida Magharibi Mhe. Elibariki Kingu alisema kamati imeona thamani ya fedha
(value for money) katika miradi ya Mahakama ambayo iko katika ubora
unaokubalika hasa katika matumizi ya fedha za wananchi.
“Majengo ni mazuri, tunampongeza Waziri wa Katiba na
Sheria pamoja na uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kazi nzuri”, alisema huku
akiongeza kuwa Mahakama ni Mhimili wa utoaji haki hivyo endapo kuna matumizi
mazuri ya fedha za Umma ni kiashiria kuwa hata haki itatendeka ndani ya majengo
hayo.
Aidha, wajumbe wa kamati hiyo pia wanatarajiwa
kutembelea na kukagua ujenzi wa majengo ya Mahakama Jumuishi (Intergrated
Justice Centre) wilayani Temeke jijini Dar es salaam na mkoani Arusha na
baadaye kutembelea Mahakama za wilaya za Chemba na Bahi mkoani Dodoma.
Mahakama ya Tanzania inaendelea na ujenzi wa majengo
ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo majengo sita ya Mahakama
Kuu Jumuishi katika miji ya Arusha, Mwanza, Dodoma, Morogoro na Dar es salaam.
Majengo mengine ni ya Mahakama za Hakimu Mkazi,
Mahakama za wilaya na Mahakama za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo
Lindi, Njombe, Katavi, Sikonge, Bahi, Chemba na Mahakama za Mwanzo kadhaa
zikiwemo Kibaigwa-Dodoma, Nyakibimbili-Bukoba, Matili-Songea, na Kimbe-Tanga.
Aidha, Mahakama imekamilisha ujenzi wa majengo mawili
ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Kigoma na Mara, Mahakama za Hakimu Mkazi katika
mikoa ya Simiyu, Geita, Pwani pamoja na Mahakama za wilaya zaidi ya 16 katika
maeneo mbalimbali nchini.
Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe likiwa katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wake.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukagua jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akieleza jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea jengo la Mahakama Kuu Jumuishi leo mkoani Morogoro.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba wakiwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (wa tano kushoto).
Jengo la Mahakama Kuu Jumuishi lililopo Morogoro linalotarajiwa kukamilika hivi karibuni
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukagua jengo hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni