· Rais Samia Aagiza Mchakato wilaya ya Chato kuwa Mkoa kukamilika
· Jaji Mkuu amuelezea kuwa kiongozi aliyekuwa na ndoto
za kuendeleza watanzania
Na Lydia Churi-Mahakama
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan ameagiza kukamilika kwa mchakato wa kuifanya wilaya ya Chato kuwa
mkoa na kusema kuwa endapo wilaya hiyo itakidhi vigezo vya kuwa mkoa Serikali
itapitisha na isipokidhi maelekezo mengine yatatolewa.
Akizungumza katika Ibada ya Mazishi ya aliyekuwa Rais
wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wilayani Chato Mhe. Samia alisema
Serikali itatekeleza ahadi zote zilizopo kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na zile alizozitoa hayati Dkt. Magufuli kwa wananchi wake.
Mhe. Samia alisema Serikali haitawaacha wananchi wa
Chato ikiwemo familia ya hayati Dkt. Magufuli. Ameishukuru familia pamoja na
ofisi binafsi ya Rais kwa ushirikiano waliotoa kwa serikali katika kipindi cha
msiba.
Alisema maono, mikakati na falsafa ya Hapa Kazi Tuu
itaendelea kuwepo na kufanyiwa kazi. Aliwataka watumishi wa Umma na Sekta
binafsi kufanya kazi kwa bidii na kuonyesha upendo na mshikamano ili
kuliendeleza taifa.
“Naungana na Spika wa Bunge katika andiko la Biblia Isaya
41:10, Mungu hatatuacha, tumwelekee yeye naye atatushika mkono, tuendelee na yale
tuliyopanga”, alisema Mhe. Rais.
Rais Samia alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na
Mwakilishi wa wazee wa Chato Mzee Samwel Bigambo alipokuwa akitoa salaam kwa
niaba ya wazee wa Chato wakati wa Ibada ya mazishi. Mzee Bigambo alikumbusha ahadi
ya kuifanya wilaya ya Chato kuwa mkoa iliyotolewa wakati wa uhai wa Rais Magufuli.
Akitoa salaam katika Ibada ya mazishi, Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemuelezea aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuwa alikuwa ni kiongozi
shupavu aliyekuwa na maono na ndoto za kuendeleza maisha ya watanzania.
Jaji Mkuu alisema Mhe. Magufuli alikuwa ni moja ya
viongozi wa Afrika wenye maono ya mbali na aliyejali wananchi wake na kutetea
wanyonge katika kipindi cha uongozi wake alipokuwa hai.
“Hayati Rais Magufuli alikuwa ni kiongozi aliyehoji
mambo mengi ikiwa ni pamoja na kwa nini sheria na taratibu hazina kasi na
matarajio ya karne ya 21” alisema Jaji Mkuu.
Alisema Mahakama ya Tanzania ni shahidi wa ndoto na
maono aliyokuwa nayo hayati Dkt. John Pombe Magufuli na wapi alitaka kuipeleka
nchi ya Tanzania kimaendeleo. Aliongeza kuwa mwaka 2016 alisaini mkataba wa
mkopo wa shilingi bilioni 135 kutoka Benki ya Dunia uliowezesha maboresho
makubwa kufanywa na Mahakama ya Tanzania.
“Historia ya Rais Magufuli bado inajiandika na haitakamilika
mpaka pale miradi ya Mahakama iliyoanza itakapokamilika” alisema Jaji Mkuu wa
Tanzania na kuongeza kuwa lengo lilikuwa ni kukamilisha ujenzi wa majengo ya
Mahakama za Mwanzo na Mahakama Kuu zote lakini anaamini kazi hiyo itakamilika
chini ya uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Jaji Mkuu alisema Mahakama itampa ushirikiano
unaostahili Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan na anaamini Rais huyo atatimiza ndoto
alizokuwa nazo hayati Magufuli na ataifikisha Tanzania mahali inapotaka kufika
kimaendeleo.
Katika hafla hiyo, Jaji Mkuu alifikisha salaam za
rambirambi alizopokea kutoka kwa Majaji wakuu wa nchi kadhaa zikiwamo Rwanda,
Gambia na Namibia pamoja na salaam kutoka Benki ya Dunia na Katibu Mkuu wa
chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya madola.
Wakati huo huo, Rais Mstaafu wa awamu ya pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi
amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na hayati Magufuli ya kufanikisha Serikali
kuhamia Dodoma katika kipindi cha miaka miwili. Alisema hayati Magufuli amefanya
mambo mengi makubwa kwa maendeleo ya taifa katika kipindi cha miaka mitano
pekee na kuushangaza ulimwengu.
Naye Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
amepongeza kazi iliyofanywa na hayati Magufuli enzi ya uhai wake na kuiletea
nchi maendeleo makubwa na hatimaye kuifikisha kwenye uchumi wa kati.
Alisema hayati Magufuli alikuwa ni waziri wake hodari
aliyeweza kumudu kufanya kazi vizuri katika wizara mbalimbali zikiwemo Ardhi,
Mifugo na Uvuvi pamoja na wizara ya Ujenzi na Miundombinu. Aliongeza kuwa akiwa
wizaya ya Ujenzi alifanya kazi kubwa
katika kuunganisha mikoa ya Tanzania kwa barabara za kiwango cha lami.
Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli alifariki dunia Machi 17 mwaka huu katika Hospitali ya
Mzena jijini Dar es salaam baada ya kuugua na kuzikwa Machi 26, 2021 nyumbani
kwake Chato mkoani Geita.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiweka shada la maua kwenye kaburi la aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya mazishi yake nyumbani kwake Chato mkoani Geita.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kulia) akiwa kwenye Ibada ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika nyumbani kwake Chato mkoani Geita. Wa kwanza kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye Ibada ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika nyumbani kwake Chato mkoani Geita.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa Ibada ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika nyumbani kwake Chato mkoani Geita.
Rais wa awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kwenye Ibada ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akimpa pole Mjane wa Hayati Dkt. Magufuli, mama Janeth Magufuli mara baada ya maziko ya mumewe leo wilayani Chato mkoani Geita.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni