Ijumaa, 19 Machi 2021

RAIS MPYA AWAHAKIKISHIA WATANZANIA KUWA TAIFA LIKO IMARA

 ·      Jaji Mkuu Amuapisha leo Ikulu jijini Dar es salaam

Na Lydia Churi-Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia watanzania kuwa Taifa liko imara na viongozi wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaendeleza mazuri yote yaliyofanywa na Hayari John Pombe Magufuli.   

Rais ameyasema hayo leo mara baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Ikulu jijini Dar es salaam.

Alisema Tanzania ni nchi yenye hazina nzuri ya uongozi na misingi imara ya utaifa, udugu, umoja, ustahimilivu na nidhamu ya vyombo vya ulinzi na usalama iliyojengwa na waasisi wa taifa hili wakiwemo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

“Niwahakikishie watanzania kuwa hakuna jambo litakaloharibika”, alisema Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Rais pia aliwashukuru viongozi wa Mihimili ya Bunge na Mahakama kwa mshikamano waliouonesha katika kipindi hiki cha majonzi na maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais Mhe. Magufuli. Mhe. Samia pia alimshukuru Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano aliouonesha katika kipindi hiki.

Amewaomba watanzania kusimama pamoja na kushikamana katika kipindi hiki cha maombolezo, kuwa wamoja kama Taifa na kuacha tofauti zao na badala yake wafarijiane na kuonesha upendo, udugu na kudumisha amani ya nchi.

“Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka, bali kwa matumaini na kujiamini, si wakati wa kutazama yaliyopita bali kutazama yajayo, ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele ili kujenga Tanzania mpya ambayo Rais Magufuli aliitamani.”, alisema Mhe. Samia.

Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alifariki dunia siku ya Jumatano Machi 17, 2021 jijini Dar es salaam baada ya kuugua. Kufuatia msiba huo, Serikali imetangaza siku 21 za maombolezo ambapo bendera ya Taifa itakuwa ikipepea nusu mlingoti.

Mwili wa Hayati Rais Magufuli utaagwa jijini Dar es salaam Machi 20 na 21 na kupelekwa jijini Dodoma ambapo utaagwa Jumatatu Machi 22 na kusafirishwa kwenda kwao wilayani Chato ambapo familia, ndugu na wananchi watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kwa mpendwa wao. Mwili wa Rais Magufuli utazikwa kwa heshima zote siku ya Jumatano Machi 25, 2021 nyumbani kwao Chato mkoani Geita.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimuapisha Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Ikulu jijini Dar es salaam. 

Mhe. Samia Suluhu akiapa mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo Ikulu jijini Dar es salaam. 

Mhe. Samia Suluhu Hassan akielekea kukagua Gwaride Maalum mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Ikulu jijini Dar es salaam. 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Watanzania mara baada ya kuapishwa leo Ikulu jijini Dar es salaam. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akijiandaa kukagua gwaride maalum
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini hati ya kiapo mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Ikulu jijini Dar es salaam. 

(Picha na Mary Gwera-Mahakama) 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni