Jumatatu, 31 Mei 2021

UADILIFU IWE NGUZO KUU KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YENU– JAJI MKUU

Na Innocent Kansha – Mahakama Lushoto

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewasisitiza Majaji wapya kuwa na uadilifu na maadili mema ili kuwawezesha kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba na masharti ya viapo.

Akizindua rasmi Mafunzo elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Mahakama Kuu Zanzibar mnamo Mei 31, 2021, Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha maneno aliyoyasema mara baada ya Majaji hao kuapishwa Ikulu Jijini Dar es salaam mnamo Mei 17, 2021.

"Watu husahau kuwa mara nyingi sheria sio mbaya bali ni nafsi, maadili na tabia za wanaotekeleza sheria hizo. Hivyo nawakumbusha kila jalada utakalokuwa ukilitolea uamuzi ukumbuke kuwa linagusa watu halisi, linagusa uhuru wao, biashara zao, mali zao na familia zao. Kumbukeni kuwa wananchi kupitia katiba wametupa sisi Majaji mamlaka ya utoaji haki lakini wananchi wamebaki na haki zao zote za msingi”, alisistiza Profesa Juma

Jaji Mkuu alisema Uongozi wa Mahakama ulianzisha utaratibu wa mafunzo elekezi baada ya kuona kuwa shughuli za Jaji zinagusa mali, uhai na hata maisha ya watu wengine kwa hiyo mafunzo elekezi yatawasaidia Majaji wapya wasifanye makosa yanayoweza kuepukika”, aliongeza Jaji Mkuu.

Profesa Juma alisema Mafunzo haya yatahakikisha kuwa Majaji wote mnavuka kwa haraka kipindi cha kujifunza kazi za ujaji na mnaanza mara moja majukumu yenu ya ujaji mahakamani mara baada ya zoezi hilo.

Mahakama ya Tanzania inatambua kuwa kadri dunia inavyopitia mageuzi makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia kupitia mapinduzi ya nne ya viwanda, hugusa sana taratibu zilizopo za utoaji haki.

Majaji na Mahakimu wasipopata mafunzo endelevu mara kwa mara watajikuta wanaachwa mbali sana na mageuzi ya kimaboresho. Hivyo basi mafunzo elekezi na endelevu kwa Majaji na Mahakimu ili kuboresha ufanisi, ujuzi na uwazi, aliongeza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu Prof. Juma alisema kanuni za maadili zitawalazimisha Waheshimiwa Majaji kupunguza marafiki na kujitoa kwenye mambo mengi ya kijamii kama vile makundi ya whatsapp, washirika wa kibiashara na starehe ambazo zinaweza kutia doa namna wananchi wa kawaida wanavyowategemea.

 Aidha, Kanuni za maadili zitawataka mjizuie kuonyesha hisia za wazi wazi kwa mfano, timu ya mpira unayoipenda inapopata goli, jamii haitegemei Mheshimiwa Jaji utavua shati lako na kulipeperusha hewani kwa furaha na bashasha, aliongeza Jaji Mkuu.

“Sifa yako ya Uongozi kama Jaji itajionyesha wakati wa kusikiliza na kuongoza mahakama yako. Uongozi wako mahakamani ni pamoja na kuhakikisha kuwa unapokuwa mahakamani ni kutomvunjia heshima mtu yeyote, usimdhalilishe mtu awe ni wakili, shahidi, Mshtakiwa, mtumishi wa Mahakama na hata Jaji mwenzio”, aliongeza Jaji Mkuu.

Nafasi ya Jaji kama kiongozi hujitokeza katika kutafsiri Katiba, sheria na misingi yake kwa manufaa ya ustawi wa wananchi. Mkiwa Viongozi katika tasnia ya sheria, ni lazima tafsiri zenu za Katiba na sheria zijielekeze kwenye ustawi ustawi na maendeleo ya wananchi maskini.

Jaji Mkuu aliwakumbusha Waheshimiwa Majaji kuwa sheria nyingi zimejiingiza sana katika shughuli za kila siku za kiuchumi, kibiashara, kijamii, kisiasa na kugusa maisha ya kawaida ya wananchi wengi. Hivyo Majaji kama watafsiri wa mwisho wa hizo sheria, mnatakiwa kuwa watu wa Mungu ili kuhakikisha kuwa mamlaka ambayo wananchi wamejibakizia kwa mujibu wa Katiba hayaingiliwi na Mihimili ya mitatu ya dola.

Wakati wa usikilizaji wa mashauri Jaji utakutana na sheria zenye milolongo ya hatua nyingi za kisheria ambazo ni vyanzo vya ucheleweshaji wa haki. Jaji hutakiwi kuzungumza nje ya maamuzi yako, unaweza elekeza mapungufu hayo kama mawazo yako ndani ya uamuzi wako.

Aidha, wakati mwingine Jaji unaweza kufikisha mapungufu uliyoyaona kwa Jaji Kiongozi au Jaji Mkuu ambao watayafikisha kwenye Kamati ya Kanuni ya Jaji Mkuu na hatimaye kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kujulishwa, alisisitiza Jaji Mkuu Prof, Juma.  

Wakati huo huo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi aliwapongeza Majaji wapya wa mahakama zote mbili na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kwa kuona uhitaji mkubwa iliyokuwa nao Mahakama katika eneo la rasilimali watu katika kada husika na kufanya uteuzi stahiki.

“Ni imani yangu kuwa nguvu kazi hii kubwa iliyopatikana itasaidia kufanikisha nguzo zote tatu za Mpango Mkakati wa Mahakama wa miaka mitano 2020/2021 hadi 2024/2025 uliozinduliwa mnamo Mei 21,2021 kuendeleza maboresho ya Mahakama yaliyokuwepo kwenye Mpango Mkakati wa Mahakama wa 2015/2016 hadi 2020/2021 uliofikia ukomo wa muda wake, Mimi nakuahidi kuwasimamia vyema Waheshimiwa Majaji wote waliopo Mahakama Kuu ili kutuwezesha kupata matokeo chanya na ya kushangaza ndani ya miezi sita ijayo”, alieleza Jaji Kiongozi.



 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Akizindua rasmi Mafunzo elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar (hawapo pichani). Mafunzo hayo yameanza leo tarehe 31/05/2021 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.


Jaji Kiongozi wa Makama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar ambao hawapo pichani wakati wa ufunguzi wa Mafunzo elekezi.   Baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakati wa uzinduzi wa Mfunzo elekezi.

  Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasilisha mada wakati wa mafunzo elekezi kwa Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yanayoendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani wanaoshiriki katika Mafunzo elekezi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto


 Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania wanaoshiriki katika Mafunzo elekezi yanayoendelea Chuoni hapo.
 Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar wanaoshiriki katika Mafunzo elekezi yanayoendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
 Meza Kuu wakiwa katika picha pamoja na baadhi ya wanachama wa chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wanaoshiriki katika Mafunzo elekezi yanayoendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Picha na Ibrahim Mdachi na Innocent Kansha


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni