Na Festo Sanga, Mahakama-Kigoma
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Ilvin Mugeta amezindua
rasmi kamati ya Nidhamu kwa watumishi wasio Maafisa wa Mahakama ili
kushughulikia masuala ya kimaadili kwa watumishi wa Kanda hiyo.
Akizindua
rasmi Kamati hiyo Juni mosi, 2021, Mhe. Jaji Mugeta alisema kuwa awali masuala
yote ya nidhamu yalikuwa
yanashughulikiwa makao makuu ambapo jukumu la kanda lilikuwa ni kukusanya
taarifa na kuzituma makao makuu ambao wao walikuwa na jukumu la kutoa maelekezo
kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa Umma.
Aliongeza
kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa mamlaka iliyokabidhiwa chini ya kifungu
cha 33(1) cha Sheria ya uendeshaji wa Mahakama Na 4 ya mwaka 2011 imekasimu
sehemu ya jukumu la usimamizi wa nidhamu kwa watumishi wasio maofisa wa
Mahakama kwa kamati zilizoundwa katika ngazi ya makao makuu, Mahakama Kuu Masjala
Kuu, Kanda na Divisheni zilizoanzishwa chini ya kanuni ya 19(1) (a) na (b) ya
kanuni za uendeshaji wa Mahakama.
“Nidhamu
ya watumishi ni eneo muhimu sana kwenye kuwezesha utumishi wa Umma kuwa na utumishi
wenye tija. Nidhamu na maadili vikivurugwa basi huduma kwa wananchi zitakuwa
duni. Hivyo tunaitegemea kamati yenu
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, weledi na kwa kuzingatia sheria ili
kuepusha manung’uniko ya kuonea au kupendelea watu ili hatimaye haki
itakayokuwa ikipatikana katika kamati hii iwe ni haki dhahiri” alisema Jaji
Mugeta
Naye
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka aliainisha majukumu
ya kamati hiyo kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Mahakama kuwa ni pamoja na
kufanya uchunguzi wa awali ili kubaini ukweli (facts) wa kosa ambalo mtumishi
anatuhumiwa kulitenda, kumfungulia mashtaka au kutoa adhabu ikiwa mazingira
yanaruhusu kufanya hivyo na kuunda kamati ya uchunguzi (Inquiry committee)” .
Baada
ya kamati kuzinduliwa, imeanza kazi
rasmi kwa kushughulikia shauri moja la kinidhamu lililofikishwa mbele ya kamati.
Aidha kamati imejipanga kuhakikisha inatoa elimu kwa watumishi kabla hawajafikishwa
mbele ya kamati.
Maboresho yanayoendelea ndani ya Mahakama hususani ushushaji wa baadhi ya majukumu katika ngazi mbalimbali yanalenga kuboresha huduma na kuimarisha usimamizi wa rasilimali watu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Ilvin Claud Mugeta akielezea jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kamati ya Nidhamu Kanda ya Kigoma uliofanyika Juni 1, 2021 huku wajumbe wa kamati hiyo wakifuatilia kwa makini.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka (aliyesimama mwenye suti nyeusi) akifanya utambulisho wa wajumbe wa kamati ya Nidhamu mbele ya mgeni rasmi ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Baadhi wa wajumbe wa Kamati ya Nidhamu kanda ya Kigoma wakifuatilia mada ilitolewa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Bw. Moses Mashaka (wa kwanza kushoto).
Majadiliano yakiendelea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni