Na Lydia Churi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
amewataka Mahakimu Wakazi Wafawidhi kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwenye shughuli
mbalimbali za Mahakama ikiwemo usikilizaji wa mashauri.
Akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi hati za uteuzi
Mahakimu wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Musoma na Simiyu jana
jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu aliwataka Mahakimu hao kufanya shughuli zao
nyingi kwa kutumia Tehama ili kurahisisha na kuboresha utendaji wao wa kazi.
“Matumizi ya Tehama ni moja ya eneo linalotakiwa
kutubadilisha sisi katika utendaji wetu wa kazi, hivyo kuweni mstari wa mbele ili
kufanikisha Mahakama Mtandao”, alisema Jaji Mkuu.
Aidha Jaji Mkuu amewashauri Mahakimu walioapishwa
kutumia Teknolojia hiyo katika kutatua changamoto watakazokutana nazo kwenye
utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ikiwemo ile ya upungufu wa watumishi
wa kada mbalimbali mahakamani.
Jaji Mkuu pia amewashauri Mahakimu hao kujenga tabia
ya kujisomea hasa nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania
pamoja na Tume ya Utumishi wa Mahakama ili wawe na uelewa mpana utakaowawezesha
kuwaelimisha watumishi watakaowaongoza masuala mbalimbali ya kimahakama.
“Mahakama ina nyaraka nyingi, someni, eleweni,
chambueni na kuzisambaza kwa watumishi walio chini yenu ili dhana ya maboresho
ya huduma za Mahakama ieleweke na kufahamika kwa wanachi wengi zaidi”,
alisisitiza Jaji Mkuu.
Alisema pamoja na majukumu mengine waliyonayo,
Mahakimu Wafawidhi wote hawana budi kuwa mstari wa mbele katika kusimamia kwa
umakini utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama pamoja na
program ya maboresho ya huduma za Mahakama katika maeneo yao ya kazi.
Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania
Bw. Mathias Kabunduguru amewataka Mahakimu hao kutenda haki wanaposikiliza
mashauri ya aina yote ili kujenga imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama na
kushirikiana vizuri na viongozi wa Serikali katika maeneo yao.
Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert
Chuma amewataka Mahakimu hao kusimamia suala la maadili kwa watumishi
wanaowaongoza na kuhakikisha wanabuni mikakati mbalimbali itakayowezesha
kumalizika kwa mlundikano wa mashauri mahakamani.
Mahakimu Wakazi waliokabidhiwa hati za uteuzi na Mhe.
Jaji Mkuu ni Mhe. Frank Mushi aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
wilaya ya Kinondoni ambaye sasa anakuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Musoma. Mwingine ni Mhe. Judith Kamala aliyekuwa Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Same na sasa ameteuliwa kuwa Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi Wafawidhi mara baada ya
kuwakabidhi hati za uteuzi. Kushoto ni Mhe. Frank Mushi (Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma) na kulia ni Mhe. Judith Kamala (Hakimu
Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu).
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi hati ya uteuzi Mhe. Judith Kamala (Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu).
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama ya Tanzania mara baada ya kuwakabidhi hati ya uteuzi Mahakimu Wakazi Wafawidhi. Wa tatu kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni