Na Mary Gwera, Mahakama
Mradi
wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (Integrated Justice Centre) unaojengwa
jijini Arusha unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, 2021 huku
ikielezwa kuwa kwa sasa umefikia asilimia 83 ya ujenzi wake.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari wa mkoani Arusha katika ziara maalum ya kutembelea mradi
huo iliyofanyika mapema leo Juni 04, 2021, Mhandisi wa Mahakama ya Tanzania, Bw.
Fabian Kwagilwa alisema kuwa kwa sasa Mkandarasi yupo katika hatua ya
umaliziaji wa jengo ‘finishing stage’.
“Utekelezaji
wa mradi huu ulianza mwezi Januari 2020, ambapo mpaka sasa umekamilika kwa asilimia
83, na mradi huu unagharimu fedha za kitanzania zenye thamani ya takribani
shilingi bilioni 8.293,” alisema Mhandisi Kwagilwa.
Alisema
kuwa mradi huu ni moja kati ya miradi sita (6) ya ujenzi inayoendelea kujengwa
na Mahakama ya Tanzania katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Mwanza na Dar es
Salaam ambapo yote inalenga kuwafikishia wananchi huduma ya upatikanaji wa haki
kwa urahisi zaidi.
Aliongeza
kuwa katika jengo hilo kutakuwa na ngazi zote za Mahakama kwa maana ya Mahakama
ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu.
Kwa
upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna amesema
kuwa ujenzi wa jengo hilo na mengineyo ya Mahakama yawe ni chachu kwa Watumishi
wa Mahakama kuendelea kuchapa kazi.
“Niseme
kwamba, Mhe. Jaji Mkuu amesisitiza na mimi hili lazima niliseme kuwa Majengo
haya ambayo Mahakama inajenga iwe ni chachu kwa sisi Watumishi kufanya kazi kwa
ufanisi zaidi ili kuongeza Imani ya wananchi kwa Mahakama,” alieleza.
Aliongeza
kuwa kupatikana kwa jengo hilo kutasaidia pia kupatikana kwa nafasi kuwa zaidi
ambayo itawezesha kufanya kazi katika eneo kubwa zaidi tofauti na ilivyo sasa
katika jengo la Mahakama Kuu kanda ya Arusha wanalotumia.
Mbali
na hayo, Mhe. Jaji Mzuna alisema faida nyingine ya jengo hilo litawawezesha
wananchi kupata huduma ya haki katika eneo moja kwa urahisi zaidi badala ya
kusafiri umbali mrefu kutafuta haki zao.
“Wananchi
wana kiu ya kufungua mashauri kwa sababu wanajua haki zao, hiki ni kitu kizuri
badala ya kujichukulia sheria mkononi, na vilevile wana Imani na Mahakama hivyo
itasaidia kushughulikia mashauri kwa muda mfupi na haraka zaidi,” alisema.
Mahakama ya
Tanzania kwa sasa inaendelea kuboresha miundombinu yake kwa
kukarabati majengo ya zamani na kujenga mengine mapya, hivi karibuni
inatarajia kuanza ujenzi wa majengo 25 ya Mahakama za wilaya katika maeneo
mbalimbali nchini yasiyokuwa na huduma ya Mahakama za wilaya.
Kupitia Mpango
wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu (Five Year Infrastructural
Development Plan) 2016/2017-2020/2021 unaohusu ujenzi na ukarabati wa majengo
ya Mahakama, maeneo ya kipaumbele yaliainishwa kwa kuzingatia vigezo vya
idadi ya Watu, wingi wa mashauri, maeneo mapya ya utawala, umbali kwa wananchi
kufuata huduma shughuli za kiuchumi, na mazingira ya kijiografia.
Mradi huu ya ujenzi
wa kituo Jumuishi cha utoaji Arusha unatekelezwa na Mkandarasi ‘LIJUN
DEVELOPMENT CONSTRUCTION CO. LTD’ chini ya usimamizi wa Mkandarasi Mshauri ‘HAB
CONSULT LTD.’
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni