Na Innocent Kansha – Mahakama Lushoto.
Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman amewataka Majaji wapya wa
Mahakama Kuu ya Tanzania kuongeza uwazi, uwajibikaji, kujenga utamaduni wa
kufikika na kutoa maamuzi kwa wakati na kwa kushirikiana na wadau.
Akizungumza na Majaji
wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania alipowatembelea wakati wa mafunzo elekezi katika
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto mnamo Juni 3, 2021 Jaji Mkuu Mstaafu Mhe.
Mohamed Othman aliwapongeza kwa kuteuliwa na Kuwakumbusha Majaji kuwa mwananchi
wa kawaida anatamanani kuona shauri lake linamalizika mapema ili ajue hatima
yake
“Ili Mahakama ifikie lengo hilo ni lazima tuwe
na Majaji, Mahakimu na Watumishi wa kada mbalimbali wenye weledi, wanaoaminika na
wenye sifa za uwajibikaji na uadilifu”, aliongeza Mhe. Othman
Aidha, Kila Jaji
alieteuliwa ana kipawa na karama zake mkatumie huo uwezo wenu mliobarikiwa nao
kuisaidia Mahakama ya Tanzania kuleta mabadiliko ya kweli, kila mmoja wenu kama
Kiongozi atumie maarifa yake kuisaidia Taasisi na kumsaidia Jaji Kiongozi na
Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu Msataafu Mhe.
Othman pia aliwakumbusha Majaji matumizi ya lugha sahihi wakati wa kukosoa ama
kusahihisha hukumu za mahakama za chini, tambueni kuwa hukumu au maamuzi unayoyatoa
ni kumbukumbu ya kudumu, hivyo lugha inatakiwa kuwa yenye ufasaha wa hali ya
juu.
Majaji mnatakiwa
kupambana na rushwa kwa nguvu zote ndani ya Taasisi. Muangalie suala la maadili
kwa jicho la tatu, lazimisheni maadili miongoni mwenu ili yaonekane yanatendeke
itajenga taswira chanya kwa watumishi wengine.
Jaji Chande aliwashauri
watumishi wa Mahakama kuendelea kujiendeleza kielimu kwa kusoma fani mbalimbali
ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa kila siku wa Taasisi, hii
itasaidia kuendana na kasi kubwa ya maboresho yanayoendelea mahakamani.
Mathalani, Maboresho
makubwa na ufanisi unaoonekana umetokana na kuanzishwa Tume huru ya Utumishi wa
Mahakama na pia kutenganisha kada mbili za taaluma ya watendaji na wasajili,
kwa maana ya Watendaji kushughulika na masuala ya utawala na fedha na Wasajili
kushughulika masuala ya utaratibu wa mashauri mahakamani. Mfumo huu wa
uendeshaji shughuli za kimahakama Tanzania iliiga mfumo huo kutoka Tume ya
utumishi wa Mahakama ya Jamhuri ya Ireland, aliongeza Jaji Othman.
Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumza na Majaji wapya
walio kwenye mafunzo elekezi (hawapo pichani) mara baada ya kuwatembelea mnamo Juni 3, 2021
Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar wakimsikilia
Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman alipowatembelea darasani.
Baadhi ya Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar wakimsikilia
Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman alipofanya mazunzungumzo nao.
Picha na Innocent Kansha - Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni