Na Festo Sanga, Mahakama-Kigoma
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Kigoma ambaye kwa sasa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
Mhe. Ilvin Mugeta amekabidhi ofisi kwa Jaji Mfawidhi aliyehamia Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Lameck Mlacha huku akimhakikishia Mhe. Jaji
Mlacha kuwa watumishi wa Kanda hiyo wana ari ya kufanya kazi.
Akifanya makabidhiano hayo Juni 30, 2021, Mhe. Jaji Mugeta
alimfahamisha Jaji Mlacha kuwa Kanda hiyo iliyoanzishwa mwaka 2019 ilitumia
muda wa kutosha kuwajengea uwezo
watumishi, kusimamia nidhamu na maadili na kuhakikisha kwamba kazi za wadau
zinafanyika kwa kuzingatia taratibu za kimahakama na za kisheria zilizowekwa na
kusema kuwa Kanda ni salama.
“Kanda ni salama, watumishi tuna ari ya kufanya kazi
bila kutegeana na kwa moyo wote hivyo nakukabidhi watu ambao wako tayari
kutekeleza majukumu yao kwa maelekezo ya kisheria,” alisema Jaji Mugeta.
Naye Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Kigoma, Mhe. Jaji Lameck Mlacha amewaomba ushirikiano watumishi katika utendaji
kazi na kuwaasa kila mmoja kutimiza wajibu wake katika nafasi aliyonayo.
“Tuna wajibu wa kuendelea kujituma na kufanya kazi kwa
kuzingatia weledi na kushirikiana. Nimefahamishwa juu ya Uhaba wa watumishi
uliopo hivyo wale ambao wanafanya kazi zaidi tutaendelea kutambua na kuthamini
jitihada zao ili kuwatia moyo”. Alisema Jaji Mlacha.
Mheshimiwa Jaji Mlacha amewataka watumishi kuendelea
kuzingatia maelekezo mbalimbali yanayotolewa na wataalam wa Afya juu ya namna ya
kukabiliana na ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID 19) ikiwa ni pamoja na
kuvaa barakoa, kunawa kwa maji tiririka na sabuni na kujiepusha na mikusanyiko
isiyo ya lazima.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Uongozi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Athumani Kirati wa Kanda hiyo,
amemuahidi ushirikiano wa kutosha na kusema kuwa Uongozi na watumishi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma wana imani kuwa atawavusha salama. Vilevile
alimtakia Mhe. Jaji Mugeta majukumu mema katika kituo chake kipya.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi, Bi Rhoda Kijumbe
ambaye ni katibu Mahsusi alisema kuwa Mhe.
Jaji Mugeta ameacha alama katika uongozi wake katika Kanda ya Kigoma hivyo
atakumbukwa kwa mengi mazuri na alichukua nafasi hiyo kumkaribisha Mhe. Jaji Mlacha katika Kanda ya kigoma.
Katika hafla hiyo Jaji Mugeta alimkabidhi Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kigoma taarifa ya makabidhiano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni