Jumanne, 6 Julai 2021

MAHAKAMA INA MCHANGO KATIKA UKUAJI WA UCHUMI; JAJI KIONGOZI

Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amesema hakuna nchi inayoweza kuendelea bila kuwa na Mahakama bora, hivyo, Mahakama inaendelea kuboresha huduma zake wakati wote kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa haki kwa wakati na hatimaye kuwezesha ukuaji wa uchumi wa nchi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Julai 06, 2021 alipotembea Banda la Mahakama lililopo katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa, Mhe. Jaji Kiongozi aliwahakikisha wananchi kuwa Mahakama inaendelea kusikiliza mashauri mapema na kuyatolea maamuzi ili kufikia ndoto ya uchumi wa viwanda. 

"Mwekezaji akiwa na mgogoro na akaufikisha mahakamani endapo utasikilizwa mapema na kutolewa maamuzi tutakuwa tunatengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji," alisema Dkt. Feleshi. 

Aidha, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi alishauri migogoro mbalimbali  ya biashara  kupelekwa  kwenye Kituo cha Usuluhishi  waweze kusainishana mikataba ili mashauri yaishe bila kupoteza  muda.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Kiongozi alitoa wito kwa wananchi kutembelea banda la Mahakama ili kupata elimu ya masuala mbalimbali na taratibu za kimahakama.

Huduma zinazopatikana katika banda la Mahakama ni pamoja na huduma ya Mahakama inayotembea inayosajili na kusikiliza kesi za mirathi, talaka, madai na jinai, kusikiliza baadhi ya mashauri kwa njia ya mtandao kwa kutumia Mahakama mtandao ‘virtual court’.

Nyingine ni utoaji wa elimu ya elimu juu ya taratibu mbalimbali za ufunguaji wa mashauri yakiwemo mashauri ya mirathi, namna ya kuandika wosia, kusikiliza na kutolea suluhu malalamiko ya wananchi, kutoa fomu za udahili za Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), msaada wa kisheria ‘TLS’ ikiwemo kusainiwa viapo na vivuli vya vyeti nk.

Miongoni mwa Mabanda yaliyotembelea na Mhe. Jaji Kiongozi ni pamoja na banda la Wamachinga, Banda la Zanzibar, Mahakama pamoja na Polisi.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (katikati) akiwasili katika banda la Mahakama lililopo katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba' 2021. Mhe. Jaji Kiongozi alipata fursa ya kutembelea mabanda kadhaa leo Julai 06, 2021 katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Dar es Salaam. Kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.
Mhe. Jaji Kiongozi akipata ufafanuzi kutoka kwa mmoja wa Wajasiriamali wadogo wanaoshiriki katika Maonesho ya 'Sabasaba' ndani ya banda la Wamachinga.
Mhe. Jaji Kiongozi akipata akizungumza na Mama mjasiriamali ndani ya banda la Wamachinga ambao wameshiriki kwa mara ya kwanza katika maonesho hayo.
Akipata maelezo ndani ya banda la ZANZIBAR lililopo katika Maonesho ya Sabasaba.
Mhe. Jaji Dkt. Feleshi akifurahia jambo ndani ya Mahakama inayotembea inayotoa huduma katika Maonesho hayo.
Mhe. Jaji Kiongozi akisaini kitabu cha Wageni alipotembelea banda la Chuo cha Uongozi wa Mahakama lililopo ndani ya banda la Mahakama.
Afisa kutoka Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Bi. Hamisa Tuli (kulia) akifafanua jambo kwa Mhe. Jaji Kiongozi pindi Kiongozi huyo alipotembelea Banda la Mahakama.
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (aliyenyoosha mkono) akimuonyesha Mhe. Jaji Kiongozi jinsi kesi zinavyoendeshwa moja kwa moja 'live' kupitia Mahakama mtandao 'virtual court'.
Afisa wa Polisi (kulia) akitoa maelezo kwa Mhe. Jaji Kiongozi. Jeshi la Polisi linashiriki pia katika Maonesho ya Sabasaba.
Muonekano wa Mahakama inayotembea ambayo inatoa huduma katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba' 2021.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni