Na Lydia Churi- Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
ameridhia ombi la Chama cha Mawakili Tanganyika (Tanganyika Law Society-TLS) la
wanasheria wanaokubaliwa na kupokelewa kuwa mawakili kuongezewa kiapo cha
uadilifu.
Ombi hilo lilitolewa kwa Jaji Mkuu wa Tanzania jana na
Rais wa chama hicho Prof. Edward Hosea alipomtembelea Jaji Mkuu ofisini kwake
kwa lengo la kujitambulisha na kuutambulisha uongozi mpya wa chama hicho.
“Kiapo cha uadilifu ni utaratibu unaotumika hata kwa
viongozi wengine wanapoapishwa hivyo mimi sina pingamizi, kuna haja ya kukumbushana
umuhimu wa maadili kwenye kazi za utoaji haki”, alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu alisema Chama cha Mawakili Tanganyika ni wadau
muhimu kwenye utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya
Tanzania kwa kuwa mafanikio ya mhimili huo yanatokana na mchango mkubwa
unaotolewa na chama hicho.
Kwa Upande wake, Rais wa TLS ameipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa matumizi ya Tehama pamoja na kutoa miongozo mbalimbali
inayorahisisha upatikanaji wa haki nchini.
Alisema miongozo inayotolewa na Mahakama imesaidia
kurahisisha upatikanaji wa haki huku akitolea mfano wa mwongozo kutoa adhabu
(sentencing Manual) pamoja na ule wa masuala ya dhamana.
“Chama cha Mawakili Tanganyika kitaendeleza mahusiano
mazuri yaliyopo kati yake na Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kuboresha
shughuli za utoaji haki nchini na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati”,
alisema.
Kuhusu changamoto za chama hicho, Prof. Hosea alisema
hivi sasa baadhi ya Taasisi zikiwemo za Serikali zimekuwa zikikataa viapo vya
mawakili na kuelekeza matumizi ya viapo vinavyotoka mahakamani. Aidha, alimwomba
Jaji Mkuu kukisaidia chama hicho ili viapo vya wananchama wake vikubalike kwa
wote kama ambavyo sheria imeruhusu.
Rais wa chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Prof. Edward Hosea akizungumza wakati alipomtembelea
Jaji Mkuu ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na kuutambulisha uongozi
mpya wa chama hicho. Aliyekaa katikati mbele ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akizungumza wakati Rais wa TLS alipomtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania ofisini kwake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni