Jumatano, 11 Agosti 2021

ANDAENI MAZINGIRA RAFIKI MNAPOSIKILIZA MASHAURI YA WATOTO: JAJI KIONGOZI

 Na Lydia Churi-Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewataka Majaji, Mahakimu na Mawakili kuandaa mazingira rafiki kwa Watoto wanaposikiliza mashauri yanayowahusisha watoto wakati Mahakama ikiendelea na jitihada za kuboresha miundombinu yake katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na wadau wa Mhimili huo, Jaji Kiongozi ambaye pia ni Mjumbe wa Tume hiyo alisema Sheria imetambua kuwepo kwa Mahakama za Watoto hivyo kwenye maeneo yasiyokuwa na Mahakama za Watoto, Majaji na Mahakimu hawana budi kuandaa vyumba mbadala kwa ajili ya kusikiliza mashauri ya aina hiyo.

“Mashauri yanayowahusisha Watoto yasikilizwe katika mazingira rafiki kwa mujibu wa sheria ya Mtoto ya mwaka 2011 pamoja na kanuni zake zote kama zilivyo”, alisisitiza Jaji Kiongozi.

Alisema majengo yote mapya ya Mahakama na yale yanayoendelea kujengwa nchini yamezingatia uwekwaji wa mazingira rafiki kwa Watoto kwa ajili ya kusikiliza mashauri yatakayowahusu. Aliongeza kuwa hivi sasa kuna Mahakama za Watoto katika baadhi ya maeneo nchini yakiwemo Mbeya na Kisutu jijini Dar es salaam.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi alisema suala la uanzishwaji wa Mahakama za Watoto si suala la Mahakama ya Tanzania peke yake bali ni jambo linalohusisha jamii nzima ya watanzania. Alisema Mahakama hizo zilijengwa katika maeneo machache nchini.

Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa wadau wote wa utoaji haki nchini kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili haki iweze kutendeka kwa wakati.

“Tukipenda wote kuona haki inatendeka kwa wakati, tujiepushe kwa namna yoyote ile kwa hila kufanya jambo lolote ambalo mwisho wake litasababisha haki isitendeke”, alisisitiza Prof. Kilangi.

Awali akitoa mchango wake katika kujadili masuala ya upatikanaji wa haki nchini, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Josephine Mwaipopo alisema pamoja na mafanikio ya Mahakama katika kuboresha huduma zake, bado kuna changamoto ya kukosekana kwa mazingira rafiki wakati wa kusikiliza mashauri yanayowahusisha Watoto.    

Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na ziara katika mikoa ya Iringa Njombe, Mbeya na Songwe kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu kwa wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya pamoja na wadau wa Mahakama.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume hii iliundwa kwa lengo la kusimamia mambo muhimu yanayohusu Mhimili wa Mahakama.

Baadhi ya kazi za Tume hiyo ni pamoja na kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu, kumshauri Rais kuhusu masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya Majaji, kushauri kuhusu ajira za Mahakimu na kusimamia nidhamu yao.

Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.

 

Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na wadau wa Mhimili huo jana mjini Iringa. 

Wadau wa Utoaji Haki nchini wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Tume ya Utumishi wa Mahakama jana mjini Iringa. 


 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni