· Mwanasheria Mkuu wa Serikali naye awashauri kusimamia Misingi ya Maadili
Na Lydia
Churi- Mahakama, Iringa
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka
watumishi wa Mahakama kutenda haki kwa watu wote wote pasipo kuangalia hali ya kiuchumi
ama kijamii ya Mtanzania anayefika mahakamani kutafuta haki.
Akizungumza kwenye Mkutano kati ya Tume ya Utumishi wa
Mahakama na watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Iringa, Jaji Mkuu ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Tume hiyo aliwaambia watumishi hao kuwa Katiba ya nchi imeupa
Mhimili wa Mahakama imani kubwa ya kusimamia suala la utoaji haki hivyo hawana
budi kutekeleza jukumu hilo kwa kufuata sheria.
“Tunalo jukumu kubwa la kusimamia haki na Katiba ya
nchi inatutaka kutochelewesha upatikanaji wa haki pasipokuwa na sababu za
msingi, hivyo mnapotekeleza wajibu wenu vizuri mnaipa uhai Katiba” alisema Jaji
Mkuu.
Jaji Mkuu alisema suala la utoaji haki ni sehemu
muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo inazingatia uwepo
kwa amani katika jamii, hivyo endapo watumishi wa Mahakama watatekeleza wajibu
huo kikamilifu watatoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira hiyo muhimu
kwa maendeleo ya Taifa.
Alisema Majaji na Mahakimu wanapotoa maamuzi ya kesi
kwa wakati wataiwezesha Mahakama kuchangia katika kujenga uchumi wa Taifa kwani
wananchi watapata muda zaidi wa kufanya shughuli za uzalishaji. “Tusisahau kuwa
tunapotoa haki kwa wakati tunachangia maendeleo ya Taifa letu”, alisisitiza.
Kuhusu matumizi ya Tehama, Jaji Mkuu alisema Mahakama
imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye Tehama hivyo ipo haja ya kwenda mbele zaidi
katika matumizi hayo ili kuendana na karne ya 21 ya Mapinduzi ya nne ya
viwanda. Aliongeza kuwa matumizi ya Tehama yataongeza uwazi, ufanisi na kujenga
imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.
Wakati huo huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Prof.
Adelardus Kilangi amewashauri
watumishi wote wa Mahakama nchini kufanya kazi zao kwa kusimamia misingi ya
maadili yanayotarajiwa kwao.
“Tufahamu kuwa kila wakati jamii inatutazama,
inaangalia tunavyofanya kazi hivyo fanyeni kazi kwa kuzingatia weledi, ufahamu na
kuzingatia maadili na miiko yote iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria, kanuni,
taratibu na hata mapokeo”, alisema Mwanasheria Mkuu.
Alisema endapo watumishi wa Mahakama watafanya kazi
kwa kuzingatia maadili, watatoa mchango mzuri katika maendeleo ya Taifa kwa
ujumla na kuchangia kuwa na jamii iliyo tulivu.
Kiongozi huyo pia ametoa wito kwa Kamati za Maadili za
Maafisa wa Mahakama za mikoa na wilaya kuongozwa na maadili zinapofanya kazi
yake.
Wajumbe wa Tume hiyo leo wameanza ziara katika Mkoa wa
Iringa na baadaye mikoa ya Njombe, Mbeya na Songwe kwa lengo la kuitangaza na
kutoa elimu kwa wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya pamoja na wadau
wa Mahakama.
Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa kwa mujibu wa Ibara
ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa
pamoja na Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume hii
iliundwa kwa lengo la kusimamia mambo muhimu yanayohusu Mhimili wa Mahakama.
Baadhi ya kazi za Tume hiyo ni pamoja na kumshauri
Mhe. Rais katika uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu, kumshauri Rais kuhusu
masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya Majaji, kushauri kuhusu ajira za
Mahakimu na kusimamia nidhamu yao.
Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu wa
Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa Mahakama ya
Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na
wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa pamoja na watumishi wengine wa Mahakama wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo kwenye picha) alipokuwa akifungua Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na watumishi wa kanda ya Iringa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Iringa Mhe. Dkt. John Utamwa akisoma Taarifa ya Utekelezaji ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni