Na Mary Gwera, Mahakama
Mkuu
wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Jokate Mwegelo pamoja na baadhi ya Viongozi wa Wilaya
hiyo wakiwemo Wahe. Wabunge wameonyesha kuridhishwa na jitihada za Mahakama ya
Tanzania kufuatia ujenzi wa Kituo cha Haki Jumuishi (IJC) kilichojengwa katika
Wilaya hiyo.
Agosti
05, 2021, Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Paul Ngwembe na Mhe. Ilvin Mugeta na
baadhi ya Maafisa wa Mahakama walikutana na Viongozi wa Wilaya hiyo, lengo
likiwa ni kutembelea na kuwafahamisha Viongozi hao juu ya uwepo wa jengo hilo jipya la Kituo
Jumuishi cha utoaji haki.
Wakizungumza
na Mkuu wa Wilaya ya Temeke ofisini kwake kabla ya kutembelea jengo hilo, Waheshimiwa
Majaji hao walimueleza dhumuni la kujenga jengo hilo kuwa litakuwa linahusika
na utoaji huduma ya masuala ya Mirathi, Ndoa na Watoto.
“Lengo
la Mahakama Jumuishi ni kutoa huduma ya haki katika jengo moja, na jengo hili
ni mahsusi kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Mirathi, Ndoa na Watoto,
kwakuwa hay ani masuala yanayoisumbua jamii kwa kiasi kikubwa,” alisema Mhe.
Jaji Paul Ngwembe.
Kwa
upande wake, Mhe. Jokate aliwashukuru Viongozi hao wa Mahakama kwa kuipa kipaumbele
Wilaya ya Temeke kusogeza huduma ya muhimu kwa wananchi.
“Napenda
nikiri kuwa nimefurahishwa na jengo hili maridadi kabisa, ambalo linakuja kuwa
suluhisho kwa wananchi wetu wa Wilaya ya Temeke na tunawaahidi kutoa ushirikiano,”
alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Huduma
za Mahakama katika jengo hili zinatarajiwa kuanza kutolewa hivi karibuni, na hili ni moja
kati ya majengo sita ya aina hii yanayojengwa pia Kinondoni- Dar es Salaam,
Morogoro, Dodoma, Mwanza na Arusha lengo likiwa ni kuendelea kuboresha na
kurahisisha huduma ya upatikanaji haki kwa wananchi.
Picha ya pamoja mbele ya jengo jipya la Kituo Jumuishi cha Utoaji haki-Temeke.
Mhe. Jaji Paul Ngwembe (aliyenyoosha mkono) akiwaonyesha kitu (haki pichani) katika jengo jipya la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki wilayani Temeke. Viongozi wa Wilaya hiyo wameonyesha kufurahishwa na Mahakama hiyo ambayo itaanza kutoa huduma hivi karibuni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni