Na Lydia Churi-Mahakama, Mbeya
Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kusikiliza na
kumaliza jumla ya mashauri 87,116 sawa na asilimia 98.7 ya mashauri 88,232 yaliyosajiliwa
katika ngazi zote za Mahakama katika kipindi cha Januari na Mei mwaka huu.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda
ya Mbeya wakati wa Mkutano kati ya wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na
watumishi hao, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza
watumishi wote wa Mahakama kwa utendaji kazi mzuri uliotukuka kufuatia
kusikilizwa kwa mashauri hayo.
Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume hiyo
alisema Mahakama Kuu zote nchini zimefanikiwa kumaliza mashauri kwa asilimia
98. Alisema, kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye Taarifa ya Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, mashauri 5,848 yalisikilizwa na kumalizika kwenye kanda
zote za Mahakama Kuu nchini kati ya Januari na Mei, 2021. Mashauri yaliyosajiliwa
katika kipindi hicho yalikuwa ni 5,875.
Kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Jaji Mkuu
alisema jumla ya mashauri 3,650 yalifunguliwa kati ya mwezi Januari na Mei,
2021 ambapo mashauri 4,320 yalisikilizwa na kumalizika sawa na asilimia 118.
Alisema Mahakama hizo zimepunguza mlundikano wa mashauri kwa asilimia 18.
Kuhusu Mahakama za wilaya, Jaji Mkuu alisema zimefanikiwa
kwa asilimia 96 kusikiliza na kumaliza mashauri yaliyosajiliwa kati ya mwezi
Januari na Mei mwaka huu. Jumla ya mashauri
15,598 kati ya mashauri 16,067 yaliyosajiliwa katika kipindi hicho
yalisikilizwa.
Aidha, Mahakama zote za Mwanzo zimefanikiwa kwa asilimia
98 kusikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 61,005 kati ya mashauri 61,931
yaliyosajiliwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wa Mahakama za Watoto, Jaji Mkuu alisema zimefanikiwa kwa asilimia 100 kusikiliza na kumaliza mashauri yote yaliyosajiliwa kati ya kipindi cha Januari na Mei mwaka huu. Jumla ya mashauri 332 yaliyohusu Watoto yalisikilizwa na kumalizika. Mashauri yaliyosajiliwa katika kipindi hicho yalikuwa ni 329.
Jaji Mkuu alisema licha ya mafanikio makubwa ya Mahakama
katika usikilizaji wa mashauri, bado Mhimili huo unakabiliwa na changamoto ya
kutotumika ipasavyo kwa njia ya usuluhishi katika kuamua migogoro mbalimbali kwenye
jamii. Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza matumizi
ya njia hii na endapo itatumika itasaidia kupunguza idadi ya mashauri
yanayofunguliwa mahakamani.
Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni kutokufungwa kwa
mashauri ya mirathi yanayofunguliwa. Alisema kati ya mashauri 31,461
yaliyofunguliwa kwa nchi nzima, mashauri 28,130 hayajafungwa mpaka sasa hali
inayoweza kusababisha wasimamizi wa mirathi kuendelea kufaidika na mali za
marehemu.
Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na
ziara katika mikoa ya Mbeya na Songwe kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu
kwa wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya pamoja na wadau wa
Mahakama.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akifungua Mkutano kati ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na Watumishi hao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni