Na Lydia Churi-Mahakama, Njombe
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
ametoa wito kwa wadau wa Mahakama kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao
ya msingi ambayo yanagusa suala la upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Akizungumza na wajumbe wa kamati za maadili za Maafisa
wa Mahakama za wilaya na mkoa katika ziara ya Tume mjini Njombe, Jaji Mkuu
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama amesema wadau hao
hawana budi kushirikiana na Mahakama kwa kuwa changamoto zinazoukabili Mhimili
huo ni za wadau wote.
“Kila mdau wa Mahakama anao mchango mkubwa kwenye
mnyororo wa utoaji haki hivyo hatuna budi kushirikiana ili wananchi wapate haki
kwa wakati”, alisema Jaji Mkuu.
Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.
Dkt. Eliezer Feleshi amewataka
Mahakimu wote nchini kuwa makini wakati wa kusajili mashauri na kahakikisha
wanasajili yale yenye vigezo vya kupokelewa ili kupunguza mlundikano wa kesi
mahakamani.
Aidha, Jaji Feleshi ametoa wito kwa vyombo vya
upelelezi kuharakisha upelelezi wa mashauri na kuyafikisha mahakamani yale
yenye mashiko. Aliongeza kuwa upelelezi unapochukua muda mrefu huweza
kusababisha ushahidi wake kupungua nguvu.
Akizungumzia matarajio ya Mahakama kutoka kwa wadau ni
kuona kuwa upelelezi wa mashauri unafanywa kwa kutumia ya njia za kisayansi ikiwemo
matumizi ya kipimo cha Vinasaba yaani DNA ili kuharakisha upelelezi na kupata
matokeo sahihi yatakayosaidia haki kutendeka.
Jaji Kiongozi pia ameishauri Taasisi ya kuzuia na
kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuchunguza malalamiko dhidi ya rushwa na
kuyathibitisha ili yanapofikishwa mahakamani yamalizike kwa wakati. Aidha, Dkt.
Feleshi pia ameitaka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuharakisha upelelezi wa
kimaabara ili kesi zisikae mahakamani kwa muda mrefu.
Wakati huo huo. Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Njombe ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe, Bw. Lautery
Kanoni ameiomba Mahakama ya Tanzania kuufikiria mkoa wa Njombe kuwa na Mahakama
Kuu kutokana na mkoa huo kuwa na mashauri mengi ya mauaji.
Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na
ziara katika mikoa ya Mbeya na Songwe kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu
kwa wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya pamoja na wadau wa Mahakama.
Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu wa
Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa Mahakama ya
Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na
wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza na wadau wa Mahakama katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wadau mjini Njombe.
Wadau wa Mahakama wakiwa katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama mjini Njombe.
Naibu Msajili na Mkurugenzi wa Usimamizi na Ukaguzi wa huduma za Mahakama na Maadili Mhe. Anna Magutu akizungumza katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wadau mjini Njombe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni