Magreth Kinabo na Lydia Churi- Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof, Elisante Ole
Grabiel amewataka watumishi wa Mahakama kuzingatia maadili wanapotekeleza
majukumu yao ili kuwezesha haki kupatikana kwa wote na kwa wakati.
Akizungumza na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Mahakama
ya Tanzania mara baada ya kuapishwa na kuwasili ofisini, Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha
dhamira ya Mahakama ya kuwasaidia wananchi kupata haki kwa wakati.
“Mahakama ni Taasisi kubwa iliyopewa jukumu la utoaji
haki hivyo tunayo kazi kubwa ya kuwasaidia wananchi kupata haki, na haki
ikikosekana nchi inaweza kuvurugika”, alisema Prof. Ole Gabriel.
Ametoa wito kwa watumishi wote wa Mahakama kujenga
utamaduni wa kufurahia kazi, kushirikiana na kupendana wakati wote ili waweze
kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania kwa ufanisi.
“Niwahakikishie kuwa Mpango Mkakati wa Mahakama ya
Tanzania ni moja kati ya Mipango kumi bora ya aina hiyo duniani, hivyo kazi
yetu itakuwa rahisi katika kuutekeleza”, alisema Mtendaji Mkuu huku akitoa
pongezi kwa Mahakama.
Aidha Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama ya Tanzania
aliwapongeza watangulizi wake kwa kuweka misingi imara ya utendaji kazi ndani
ya Mhimili wa Mhakama hivyo watumishi wa Mahakama hawana budi kuendeleza mazuri
yaliyoanzishwa
“Mimi Sikuja kuja hapa kuangusha torati, bali nimekuja
kuendeleza yale mazuri yaliyoanzishwa na yanayoendelea kufanyika,’’ alisema
Prof. Ole Gabriel huku akiupongeza Mhimili huo kwa hatua iliyofikia.
Prof. Elisante Ole Gabriel ni Mtendaji Mkuu wa tatu wa
Mahakama ya Tanzania tangu kuanzishwa kwa nafasi hiyo ndani ya Mhimili huo kwa
mujibu wa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011. Mtendaji Mkuu
wa Kwanza alikuwa ni Mhe. Balozi Hussein Athuman Kattanga (Sasa Katibu Mkuu
Kiongozi) ambaye alifuatiwa na Bw. Mathias Kabunduguru aliyestaafu kwa mujibu
wa sheria.
Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Grabiel akizungumza na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Mahakama ya Tanzania leo alipowasili ofisini mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es salaam.
Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Grabiel akizungumza huku baadhi ya viongozi wa Mahakama wakimsikiliza. Wa pili kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma, wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu aliyestaafu kwa mujibu wa Sheria, Bw. Mathias Kabunduguru, kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Bw. Solanus Nyimbi na kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu Mhe. Sharmilla Sarwatt.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania aliyestaafu Utumishi wa Umma Bw. Mathias Kabunduguru akizungumza wakati wa kumkaribisha Mtendaji Mkuu Mpya katika ofisi za Mahakama jijini Dar es salaam.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania aliyestaafu Utumishi wa Umma Bw. Mathias Kabunduguru akimkaribisha Mtendaji Mkuu Mpya Prof. Elisante Ole Gabriel katika ofisi za Makao Makuu ya Mahakama na Mahakama ya Rufani jijini Dar es salaam.
Wakuu wa Idara na Vitengo wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Grabiel mara baada ya kuzungumza nao.
Watumishi wa ofisi ya Mtendaji Mkuu wakimpokea Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Grabiel ofisini kwake alipowasili leo mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es salaam.
(Picha na Lydia Churi na Mary Gwera- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni