· Aahidi kushughulikia changamoto ya Magereza nchini
Na
Mary Gwera, Mahakama
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan ameahidi
kushughulikia changamoto ya Magereza nchini.
Akizungumza
leo Agosti 21, 2021 Ikulu Dar es Salaam mara baada ya kumuapisha rasmi Mtendaji Mkuu mpya wa
Mahakama ya Tanzania pamoja na Mabalozi wapya, Rais Samia alisema kuwa Magereza
zina hali mbaya.
“Suala
la changamoto ya Magereza nchini kama alivyotangulia kulizungumzia Mhe. Jaji
Mkuu lipo, na sisi Serikali tumesikia na tunaahidi kulifanyia kazi,” alisema Mhe.
Samia.
Kwa
upande mwingine, Mhe. Rais Samia amewataka Viongozi wote aliowaapisha kufanya
kazi kwa bidii, maarifa, weledi na nidhamu ya hali ya juu kwakuwa majukumu
yaliyopo mbele yao ni makubwa na vilevile wanategemewa na wananchi.
Akizungumzia
upande wa Mahakama, Rais Samia amemtaka Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Prof. Elisante Ole Gabriel kuendeleza maboresho ya Mahakama yaliyopo ikiwa ni pamoja
na kuboresha mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
“Mahakama
ndio mamlaka ya utoaji haki nchini, hivyo una kazi kubwa ya kuhakikisha unaendeleza
maboresho ili kuwezesha huduma ya utoaji haki inatolewa kwa wakati,”
alisisitiza.
Kwa
upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ameeleza azma ya
Mahakama ya Tanzania ya kuwa Mahakama mtandao ifikapo mwaka 2025.
“Mhe.
Rais, napenda kushukuru kwa kututeulia Mtendaji Mkuu na nimefanikiwa kupitia wasifu
wake, hivyo ni imani yangu kuwa ataisaidia Mahakama kufikia azma yake ya kuwa
Mahakama mtandao,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.
Mhe.
Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwataka Wadau wote wa Sekta ya sheria nchini kushirikiana
pamoja na Mahakama ili kufikia Mahakama mtandao.
Hali kadhalika katika hafla hiyo, Mhe. Rais amewaapisha pia Mabalozi watatu ambao ni Lt. Jen. Yakub Hassan Mohamed kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mahmoud Thabit Kombo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia na Elsie Sia Kanza kuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
Mhe. Rais aliwataka Mabalozi hao wapya kuendeleza ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hizo, kuendeleza ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa ikiwa ni pamoja na kuendeleza diplomasia ya uchumi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni